Chapter 2
1
Palitokea manabii wa uongo kati ya watu, na vivyo hivyo walimu wa uongo
watatokea kati yenu. Watu hao wataingiza mafundisho maharibifu na kumkana Bwana
aliyewakomboa, na kwa njia hiyo watasababisha ghafla maangamizi yao wenyewe.
2 Tena
watu wengi watazifuata hizo njia zao mbaya, kwa sababu yao, wengine wataipuuza
Njia ya ukweli.
3 Kwa
tamaa yao mbaya watajipatia faida kwa kuwaambieni hadithi za uongo. Lakini kwa
muda mrefu sasa Hakimu wao yu tayari, na Mwangamizi wao yu macho!
4 Malaika
walipotenda dhambi, Mungu hakuwahurumia, bali aliwatupa katika moto wa Jehanamu
ambako wamefungwa wakingojea Siku ile ya Hukumu.
5 Mungu
hakuihurumia dunia ya hapo kale, bali alileta gharika kuu juu ya nchi ile ya
watu wasiomcha Mungu; lakini Noa ambaye alihubiri uadilifu, Mungu alimwokoa
pamoja na watu wengine saba.
6 Mungu
aliadhibu miji ya Sodoma na Gomora, akaiteketeza kwa moto, akaifanya iwe mfano
wa mambo yatakayowapata watu wasiomcha Mungu.
7
Alimwokoa Loti, mtu mwema, ambaye alisikitishwa sana na mwenendo mbaya wa watu
hao waasi.
8 Loti
aliishi miongoni mwa watu hao, na kwa siku nyingi moyo wake ulikuwa katika
wasiwasi mkuu aliposikia matendo yao maovu.
9 Kwa
hiyo, basi, Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa katika majaribu watu wanaomcha
Mungu, na jinsi ya kuwaweka waovu katika adhabu hadi Siku ile ya hukumu,
10 hasa
wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kupuuza mamlaka. Watu hao ni washupavu
na wenye majivuno, huvitukana na hawaviheshimu viumbe vitukufu vya juu.
11 Lakini
malaika, ambao wana uwezo na nguvu zaidi kuliko hao walimu wa uongo,
hawawashtaki na kuwatukana hao mbele ya Bwana.
12 Watu
hao ambao hutukana chochote kile wasichoelewa, ni sawa na wanyama wasio na
akili, ambao huzaliwa na baadaye hukamatwa na kuchinjwa! Wataangamizwa kutokana
na uharibifu wao wenyewe,
13 na
watalipwa mateso kwa mateso ambayo wameyasababisha. Furaha yao ni kufanya, tena
mchana kabisa, chochote kinachotosheleza anasa zao za mwili. Hao ni fedheha na
aibu tupu kwa jumuiya yenu wakati wanapojiunga nanyi katika karamu zenu, bali
wakifurahia njia zao za udanganyifu.
14 Macho
yao yamejaa uzinzi na uwezo wao wa kutenda dhambi hauna kikomo. Huwaongoza watu
walio dhaifu mpaka mitegoni. Mioyo yao imezoea kuwa na tamaa ya mali. Wapo
chini ya laana ya Mungu!
15
Wameiacha njia iliyonyoka, wakapotoka na kuifuata njia aliyofuata Balaamu,
mwana wa Beori, ambaye alipendelea kupata faida kwa kufanya udanganyifu,
16
akakaripiwa kwa ajili ya uovu wake. Punda ambaye hasemi alinena kwa sauti ya
binadamu, akaukomesha wazimu wa huyo nabii.
17 Watu
hao ni kama chemchemi zilizokauka, kama mawingu yanayopeperushwa na tufani;
makao yao waliyowekewa ni mahali pa giza kuu.
18 Husema
maneno ya majivuno na yasiyo na maana, na kutumia tamaa zao mbaya za kimwili
kuwatega wale ambao wamejitenga hivi karibuni na watu waishio katika
udanganyifu.
19
Huwaahidi watu wengine eti watakuwa huru, kumbe wao wenyewe ni watumwa wa
upotovu - maana mtu ni mtumwa wa chochote kile kinachomtawala.
20 Watu
waliokwisha ponyoka katika upotovu wa ulimwengu kwa kupata kumjua Bwana na
Mwokozi wetu Yesu Kristo, kisha wakakubali kunaswa na kutawaliwa tena na
upotovu huo, hali yao itakuwa mbaya zaidi kuliko awali.
21
Ingalikuwa afadhali kwao kama wasingalijua kamwe njia hiyo ya uadilifu kuliko
kujua na kisha kuiacha na kupoteza amri takatifu waliyopokea.
22 Ipo
mithali isemayo: "Mbwa huyarudia matapishi yake mwenyewe," na
nyingine isemayo: "Nguruwe aliyekwisha oshwa hugaagaa tena katika
matope!" Ndivyo ilivyo kwao sasa.
|