Chapter 3
1 Wapenzi
wangu, hii ni barua ya pili ninayowaandikia. Katika barua hizo mbili nimejaribu
kufufua fikira safi akilini mwenu kwa kuwakumbusheni mambo haya.
2 Napenda
mkumbuke maneno yaliyosemwa na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na
Mwokozi mliyopewa na mitume wenu.
3 Awali ya
yote jueni kwamba siku za mwisho watakuja watu ambao mienendo yao inatawaliwa
na tamaa zao mbaya. Watawadhihaki ninyi
4 na
kusema: "Aliahidi kwamba atakuja! Je, sasa yuko wapi? Mambo ni yaleyale
tangu babu zetu walipokufa; hali ya vitu ni ileile kama ilivyokuwa mwanzo wa
ulimwengu!"
5 Watu
hao, kwa makusudi, husahau kwamba zamani Mungu alinena, nazo mbingu na nchi
zikaumbwa. Dunia iliumbwa kutoka katika maji na kwa maji;
6 na kwa
maji hayo, yaani yale maji ya gharika kuu, dunia ya wakati ule iliangamizwa.
7 Lakini
mbingu na nchi za sasa zahifadhiwa kwa neno la Mungu kwa ajili ya kuharibiwa
kwa moto. Zimewekwa kwa ajili ya Siku ile ambapo watu wasiomcha Mungu
watahukumiwa na kuangamizwa.
8 Lakini,
wapenzi wangu, msisahau kitu kimoja! Mbele ya Bwana, hakuna tofauti kati ya
siku moja na miaka elfu; kwake yote ni mamoja.
9 Bwana
hakawii kutimiza yale aliyoahidi kama watu wengine wanavyofikiri kuwa atakawia.
Yeye ana saburi kwa ajili yenu, maana hapendi hata mmoja wenu apotee, bali
huwavuta wote wapate kutubu.
10 Siku ya
Bwana itakuja kama mwizi. Siku hiyo, mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; vitu
vyake vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia itatoweka pamoja na kila
kitu kilichomo ndani yake.
11 Maadamu
kila kitu kitaharibiwa namna hiyo, je, ninyi mnapaswa kuwa watu wa namna gani?
Mnapaswa kuishi kitakatifu na kumcha Mungu,
12
mkiingojea Siku ile ya Mungu na kuifanya ije upesi - Siku ambayo mbingu
zitateketezwa kwa moto na kuharibiwa, na vitu vyake vya asili vitayeyushwa kwa
joto.
13 Lakini
sisi, kufuatana na ahadi yake, twangojea mbingu mpya na dunia mpya ambayo
imejaa uadilifu.
14 Kwa
hiyo wapenzi wangu, mkiwa mnangojea Siku ile, fanyeni bidii kuwa safi kabisa
bila hatia mbele ya Mungu, na kuwa na amani naye.
15
Mnapaswa kuuona uvumilivu wa Bwana kuwa ni nafasi anayowapeni mpate kuokolewa,
kama Paulo ndugu yetu mpenzi alivyowaandikia akitumia hekima aliyopewa na
Mungu.
16 Hayo
ndiyo asemayo katika barua zake zote anapozungumzia suala hilo. Yapo mambo
kadhaa katika barua zake yaliyo magumu kuyaelewa, mambo ambayo watu wajinga,
wasio na msimamo, huyapotosha kama wanavyopotosha sehemu nyingine za Maandiko
Matakatifu. Hivyo wanasababisha maangamizi yao wenyewe.
17 Lakini
ninyi, wapenzi wangu, mmekwisha jua jambo hili. Basi, muwe na tahadhari msije
mkapotoshwa na makosa ya waasi, mkaanguka kutoka katika msimamo wenu imara.
18 Lakini
endeleeni kukua katika neema na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu
Kristo. Utukufu uwe kwake, sasa na hata milele! Amina.
|