Chapter 2
1 Watoto
wangu, ninawaandikieni mambo haya, kusudi msitende dhambi. Lakini, ikijatokea
mtu akatenda dhambi, tunaye mmoja ambaye hutuombea kwa Baba, ndiye Yesu Kristo
aliye mwadilifu kabisa.
2 Kristo
ndiye sadaka iondoayo dhambi zetu; wala si dhambi zetu sisi tu, bali pia dhambi
za ulimwengu wote.
3
Tukizitii amri za Mungu, basi, tunaweza kuwa na hakika kwamba tunamjua.
4 Mtu
akisema kwamba anamjua, lakini hazitii amri zake, basi mtu huyo ni mwongo, na
ukweli haumo ndani yake.
5 Lakini
mtu yeyote anayeshika neno la Mungu, huyo ndiye aliye na upendo kamili wa Mungu
ndani yake. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana naye:
6 mtu
yeyote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi
Yesu Kristo.
7 Wapenzi
wangu, amri hii ninayowaandikieni si amri mpya; ni amri ileile ya zamani
mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Amri hiyo ya zamani ni ule ujumbe mliousikia.
8 Hata
hivyo, amri hii ninayowaandikieni ni amri mpya, na ukweli wake unaonekana ndani
ya Kristo na ndani yenu pia. Maana giza linatoweka, na mwanga wa ukweli
umekwisha anza kuangaza.
9 Yeyote
asemaye kwamba yumo katika mwanga, lakini anamchukia ndugu yake, mtu huyo bado
yumo gizani.
10 Yeyote
ampendaye ndugu yake, yuko katika mwanga, na hamna chochote ndani yake
kiwezacho kumkwaza mtu mwingine.
11 Lakini
anayemchukia ndugu yake, yumo gizani; anatembea gizani, na hajui anakokwenda,
maana giza limempofusha.
12
Ninawaandikieni ninyi watoto, kwa kuwa dhambi zenu zimeondolewa kwa jina la
Kristo.
13
Nawaandikieni ninyi kina baba kwani mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo,
Nawaandikieni ninyi vijana kwa sababu mmemshinda yule Mwovu.
14
Nawaandikieni ninyi watoto, kwa sababu mnamjua Baba. Nawaandikieni ninyi kina
baba, kwa kuwa mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo. Nawaandikieni ninyi
vijana kwa sababu mna nguvu; neno la Mungu limo ndani yenu na mmemshinda yule
Mwovu.
15
Msiupende ulimwengu, wala chochote kilicho cha ulimwengu. Mtu anayeupenda
ulimwengu, upendo wa Baba hauwezi kuwamo ndani yake.
16 Vitu
vyote vya ulimwengu-tamaa mbaya za mwili, vitu wanavyoviona watu na kuvitamani,
majivuno yasababishwayo na mali-vyote hivyo havitoki kwa Baba, bali vyatoka kwa
ulimwengu.
17
Ulimwengu pamoja na vitu vyake vyote vyenye kutamanika unapita; lakini mtu
atendaye atakalo Mungu, anaishi milele.
18 Watoto,
mwisho u karibu! Mlikwisha sikia kwamba adui wa Kristo anakuja, na sasa adui
wengi wa Kristo wamekwisha fika, na hivyo twajua kwamba mwisho u karibu.
19 Watu
hao wametokea kati yetu lakini hawakuwa kweli wa kwetu na ndiyo maana
walituacha; Kama wangalikuwa wa kwetu, wangalibaki nasi. Lakini waliondoka,
wakaenda zao, kusudi ionekane wazi kwamba hawakuwa kamwe wa kwetu.
20 Ninyi,
lakini, mlipata kumiminiwa Roho Mtakatifu na Kristo, na hivyo mnaujua ukweli.
21 Basi,
nawaandikieni, si kwa kuwa hamuujui ukweli, bali kwa sababu mnaujua; na pia
mnajua kwamba uongo wowote haupatikani katika ukweli.
22 Mwongo ni nani? Ni yule anayekana kwamba Yesu ni Masiha.
Mtu wa namna hiyo ni adui wa Kristo - anamkana Baba na Mwana.
23 Maana yeyote anayemkana Mwana, anamkana pia Baba; na
yeyote anayemkubali Mwana, anampata Baba pia.
24 Basi, ujumbe ule mliousikia tangu mwanzo na ukae mioyoni
mwenu. Kama ujumbe huo mliousikia tangu mwanzo ukikaa ndani yenu, basi, mtaishi
daima katika umoja na Mwana na Baba.
25 Na ahadi aliyotuahidia sisi ndiyo hii: uzima wa milele.
26 Nimewaandikieni mambo haya kuhusu wale wanaotaka
kuwapotosha ninyi.
27 Lakini, kwa upande wenu ninyi, Kristo aliwamiminieni
Roho wake. Na kama akiendelea kukaa ndani yenu, hamhitaji kufundishwa na mtu
yeyote. Maana Roho wake anawafundisheni kila kitu na mafundisho yake ni ya
kweli, si ya uongo. Basi shikeni mafundisho ya huyo Roho na kubaki katika
muungano na Kristo.
28 Naam, watoto, kaeni ndani yake kusudi wakati
atakapotokea tuwe hodari bila kuwa na sababu ya kujificha kwa aibu Siku ya kuja
kwake.
29 Mnajua kwamba Kristo ni mwadilifu kabisa; basi, mnapaswa
kujua pia kwamba kila mtu atendaye mambo adili ni mtoto wa Mungu.
|