Chapter 3
1 Oneni basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa
watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui
sisi, kwani haumjui Mungu.
2 Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado
haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba wakati Kristo
atakapotokea, tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo.
3 Basi, kila mtu aliye na tumaini hili katika Kristo,
hujiweka safi kama vile Kristo alivyo safi kabisa.
4 Kila mtu atendaye dhambi anavunja sheria ya Mungu, maana
dhambi ni uvunjaji wa sheria.
5 Mnajua kwamba Kristo alikuja kuziondoa dhambi zetu, na
kwamba kwake hamna dhambi yoyote.
6 Basi, kila aishiye katika muungano na Kristo hatendi
dhambi; lakini kila mtu atendaye dhambi hakupata kamwe kumwona, wala kumjua
Kristo.
7 Basi, watoto wangu, msikubali kupotoshwa na mtu yeyote.
Mtu atendaye matendo maadilifu ni mwadilifu kama vile Kristo alivyo mwadilifu
kabisa.
8 Lakini atendaye dhambi ni wa Ibilisi, maana Ibilisi
ametenda dhambi tangu mwanzo. Lakini Mwana wa Mungu alikuja duniani kuiharibu
kazi ya Ibilisi.
9 Kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, maana anayo
hali ya kimungu ndani yake; hawezi kutenda dhambi kwa sababu yeye ni mtoto wa
Mungu.
10 Lakini yeyote asiyetenda mambo maadilifu, au asiyempenda
ndugu yake, huyo si mtoto wa Mungu. Hiyo ndiyo tofauti iliyoko kati ya watoto
wa Mungu na watoto wa Ibilisi.
11 Na, ujumbe mliousikia tangu mwanzo ndio huu: Tunapaswa
kupendana!
12 Tusiwe kama Kaini ambaye, kwa kuongozwa na yule Mwovu,
alimuua ndugu yake. Na, kwa nini alimuua? Kwa sababu matendo yake yalikuwa
maovu, lakini yale ya ndugu yake yalikuwa mema!
13 Basi, ndugu zangu, msishangae kama ulimwengu unawachukia
ninyi.
14 Sisi tunajua kwamba tumekwisha pita kutoka katika kifo
na kuingia katika uzima kwa sababu tunawapenda ndugu zetu. Mtu asiye na upendo
hubaki katika kifo.
15 Kila anayemchukia ndugu yake ni muuaji; nanyi mnajua
kwamba muuaji yeyote yule hana uzima wa milele ndani yake.
16 Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo
aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Nasi vilevile tunapaswa kuyatoa maisha
yetu kwa ajili ya ndugu zetu.
17 Basi, mtu akiwa na mali za hapa duniani, halafu akamwona
ndugu yake ana shida, lakini akawa na moyo mgumu bila kumwonea huruma,
anawezaje kusema kwamba anampenda Mungu?
18 Watoto wangu, upendo wetu usiwe maneno matupu, bali uwe
upendo wa kweli na wa vitendo.
19 Hivyo ndivyo tuwezavyo kuwa na hakika kwamba sisi ni
watu wa ukweli; na hatutakuwa na wasiwasi mbele ya Mungu.
20 Kwa maana, hata kama dhamiri yetu yatuhukumu, twajua
kwamba Mungu ni mkuu zaidi kuliko dhamiri, na kwamba yeye ajua kila kitu.
21 Wapenzi wangu, kama dhamiri yetu haina lawama juu yetu,
basi, twaweza kuwa na uthabiti mbele ya Mungu,
22 na twaweza kupokea kwake chochote tunachoomba, maana
tunazitii amri zake na kufanya yale yanayompendeza.
23 Na, amri yake ndiyo hii: Kumwamini Mwanae Kristo, na
kupendana kama alivyotuamuru.
24 Anayezitii amri za Mungu anaishi katika muungano na
Mungu na Mungu anaishi katika muungano naye. Kwa njia ya Roho ambaye Mungu
ametujalia, sisi twajua kwamba Mungu anaishi katika muungano nasi.
|