Chapter 4
1 Wapenzi wangu, msimsadiki kila mtu asemaye kwamba ana
Roho wa Mungu, bali chunguzeni kwa makini kama huyo mtu anaongozwa na Roho wa
Mungu au la, Maana manabii wengi wa uongo wamezuka ulimwenguni.
2 Hii ndiyo njia ya kujua kama mtu anaongozwa na Roho wa
Mungu: Kila anayekiri kwamba Kristo alikuja, akawa binadamu, mtu huyo anaye
Roho wa Mungu.
3 Lakini mtu yeyote asiyemkiri Kristo hivyo, hana huyo Roho
atokaye kwa Mungu. Mtu huyo ana roho ambaye ni wa Adui wa Kristo; nanyi
mlikwisha sikia kwamba anakuja, na sasa tayari amekwisha wasili ulimwenguni!
4 Lakini ninyi, watoto, ni wake Mungu na mmekwisha washinda
hao manabii wa uongo; maana Roho aliye ndani yenu ana nguvu zaidi kuliko roho
aliye ndani ya hao walio wa ulimwengu.
5 Wao husema mambo ya ulimwengu, nao ulimwengu huwasikiliza
kwani wao ni wa ulimwengu.
6 Lakini sisi ni wake Mungu. Mtu anayemjua Mungu
hutusikiliza, mtu asiye wa Mungu hatusikilizi. Basi, kwa njia hiyo tunaweza
kutambua tofauti kati ya Roho wa ukweli na roho wa uongo.
7 Wapenzi wangu, tupendane, maana upendo hutoka kwa Mungu. Kila mtu aliye na upendo ni mtoto wa
Mungu, na anamjua Mungu.
8 Mtu
asiye na upendo hamjui Mungu, maana Mungu ni upendo.
9 Na Mungu
alionyesha upendo wake kwetu kwa kumtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, ili tuwe
na uzima kwa njia yake.
10 Hivi
ndivyo upendo ulivyo: si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, bali
kwamba yeye alitupenda hata akamtuma Mwanae awe sadaka ya kutuondolea dhambi
zetu.
11 Wapenzi
wangu, ikiwa Mungu alitupenda hivyo, basi, nasi tunapaswa kupendana.
12 Hakuna
mtu aliyekwisha mwona Mungu kamwe; lakini kama tukipendana Mungu anaishi katika
muungano nasi, na upendo wake unakamilika ndani yetu.
13 Tunajua
kwamba tunaishi katika umoja na Mungu, naye Mungu anaishi katika umoja nasi,
kwani yeye ametupa Roho wake.
14 Sisi
tumeona na kuwaambia wengine kwamba Baba alimtuma Mwanae awe Mwokozi wa ulimwengu.
15 Kila
mtu anayekiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu anaishi katika muungano na
mtu huyo, naye anaishi katika muungano na Mungu.
16 Basi,
sisi tunajua na tunaamini upendo alio nao Mungu kwetu sisi. Mungu ni upendo, na
kila mtu aishiye katika upendo, anaishi katika muungano na Mungu, na Mungu
anaishi katika muungano naye.
17 Upendo
umekamilika ndani yetu kusudi tuweze kuwa na ujasiri Siku ile ya Hukumu; kwani
maisha yetu hapa duniani ni kama yale ya Kristo.
18 Palipo
na upendo hapana uoga; naam, upendo kamili hufukuza uoga wote. Basi, mtu mwenye
uoga hajakamilika bado katika upendo, kwani uoga huhusikana na adhabu.
19 Sisi tuna upendo kwa sababu Mungu alitupenda kwanza.
20 Mtu akisema kwamba anampenda Mungu, hali anamchukia
ndugu yake, huyo ni mwongo. Maana mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona,
hawezi kumpenda Mungu ambaye hamwoni.
21 Basi, hii ndiyo amri aliyotupa Kristo: Anayempenda Mungu
anapaswa pia kumpenda ndugu yake.
|