2 John
Chapter 1
1 Mimi
Mzee nakuandikia wewe Bimkubwa mteule, pamoja na watoto wako ninaowapenda
kweli. Wala si mimi tu ninayewapenda, bali pia wote wanaoujua ule ukweli
wanawapenda ninyi,
2 kwa sababu ukweli unakaa nasi milele.
3 Neema na huruma na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa
Yesu Kristo, Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika ukweli na upendo.
4 Nilifurahi sana kuona kwamba baadhi ya watoto wako
wanaishi katika ukweli kama Baba alivyotuamuru.
5 Basi, Bimkubwa, ninalo ombi moja kwako: tupendane. Ombi
hili si amri mpya, bali ni amri ileile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo.
6 Upendo maana yake ni kuishi kwa kuzitii amri zake Mungu.
Amri niliyoisikia tangu mwanzo ndiyo hii: mnapaswa nyote kuishi katika upendo.
7 Wadanganyifu wengi wamezuka duniani, watu ambao hawakiri
kwamba Yesu Kristo amekuja kwetu akawa binadamu. Mtu asemaye hivyo ni
mdanganyifu na ni Adui wa Kristo.
8 Basi, jihadharini ninyi wenyewe ili msije mkapoteza kile
mlichokishugulikia, bali mpate tuzo lenu kamili.
9 Asiyezingatia na kudumu katika mafundisho ya Kristo, bali
anayakiuka, hana Mungu. Lakini anayedumu katika mafundisho hayo anaye Baba na
Mwana.
10 Basi, kama mtu akija kwenu bila kuwaleteeni mafundisho
hayo, msimkaribishe nyumbani kwenu, wala msimsalimu.
11 Maana anayemsalimu mtu huyo, anashirikiana naye katika
matendo yake maovu.
12 Ninayo mengi ya kuwaambieni lakini sipendi kufanya hivyo
kwa karatasi na wino; badala yake, natumaini kuwatembeleeni na kuzungumza nanyi
ana kwa ana, ili furaha yetu ikamilike.
13 Watoto wa dada yako mteule wanakusalimu.
|