Revelation
Chapter 1
1 Hizi ni
habari za mambo ambayo yalifunuliwa na Yesu Kristo. Mungu alimpa Kristo ufunuo
huu ili awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo yanapaswa kutukia karibuni.
Kristo alimtuma malaika wake amjulishe Yohane, mtumishi wake, mambo hayo,
2 naye
Yohane, ameyasema yote aliyoyaona. Na hii ndio taarifa yake kuhusu ujumbe wa
Mungu na ukweli uliofunuliwa na Yesu Kristo.
3 Heri
yake mtu anayesoma kitabu hiki; heri yao wale wanaosikiliza maneno ya ujumbe
huu wa kinabii na kushika yaliyoandikwa humu, maana wakati umekaribia ambapo
mambo haya yatatukia.
4 Mimi
Yohane nayaandikia makanisa yaliyoko mkoani Asia. Nawatakieni neema na amani
kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na anayekuja; na kutoka kwa roho saba
walio mbele ya kiti chake cha enzi,
5 na
kutoka kwa Yesu Kristo, shahidi mwaminifu, wa kwanza kufufuliwa kutoka wafu, na
ambaye ni mtawala wa wafalme wa dunia. Yeye anatupenda, na kwa damu yake
ametufungua kutoka vifungo vya dhambi zetu,
6 akatufanya
sisi kuwa ufalme wa makuhani, tumtumikie Mungu, Baba yake. Kwake Yesu Kristo
uwe utukufu na nguvu, milele na milele! Amina.
7 Tazama!
Anakuja katika mawingu! Kila mtu atamwona, hata wale waliomchoma. Makabila yote
duniani yataomboleza juu yake. Naam! Amina.
8
"Mimi ni Alfa na Omega," asema Bwana Mungu Mwenye Uwezo, aliyeko,
aliyekuwako na anayekuja.
9 Mimi ni
Yohane, ndugu yenu; na kwa kuungana na Kristo nashiriki pamoja nanyi katika
kustahimili mateso yanayowapata wale walio wa Utawala wake. Mimi nilikuwa
kisiwani Patmo kwa sababu ya kuhubiri ujumbe wa Mungu na ukweli wa Yesu.
10 Basi,
wakati mmoja, siku ya Bwana, nilikumbwa na Roho, nikasikia nyuma yangu sauti
kubwa kama sauti ya tarumbeta.
11 Nayo
ilisema, "Andika katika kitabu yote unayoyaona, ukipeleke kwa makanisa
haya saba: Efeso, Smurna, Pergamoni, Thuatira, Sarde, Filadelfia na
Laodikea."
12 Basi,
nikageuka nimwone huyo aliyesema nami, nikaona vinara vya taa saba vya dhahabu,
13 na
katikati yake kulikuwa na kitu kama mtu, naye alikuwa amevaa kanzu ndefu na
ukanda wa dhahabu kifuani.
14 Nywele
zake zilikuwa nyeupe kama pamba safi, kama theluji; macho yake yalimetameta
kama moto;
15 miguu
yake iling`aa kama shaba iliyosafishwa katika tanuru ya moto na kusuguliwa, na
sauti yake ilikuwa, kama sauti ya poromoko la maji.
16 Katika
mkono wake wa kulia, alikuwa na nyota saba, na kinywani mwake mlitoka upanga
wenye makali kuwili. Uso wake uling`aa kama jua kali.
17 Basi,
nilipomwona tu, nilianguka mbele ya miguu yake kama maiti. Lakini yeye akaweka
mkono wake wa kulia juu yangu, akasema, "Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa
mwisho.
18 Mimi ni
yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini, tazama, sasa ni mzima milele
na milele. Ninazo funguo za kifo na Kuzimu.
19 Basi, sasa andika mambo haya unayoyaona, mambo yanayotukia
sasa na yale yatakayotukia baadaye.
20 Siri ya nyota zile saba ulizoziona katika mkono wangu wa
kulia, na siri ya vile vinara saba vya taa hii: zile nyota saba ni malaika wa
makanisa; na vile vinara saba vya taa ni makanisa saba.
|