Chapter 2
1 "Kwa malaika wa kanisa la Efeso andika hivi:
"Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye ashikaye nyota saba katika mkono wake wa
kulia, na ambaye hutembea katikati ya vinara saba vya taa vya dhahabu.
2 Najua mambo yako yote; najua bidii yako na uvumilivu
wako. Najua kwamba huwezi kuwavumilia watu waovu, na kwamba umewapima wale
wanaojisemea kuwa mitume na kumbe sio, ukagundua kwamba ni waongo.
3 Wewe unayo saburi, umestahimili taabu nyingi kwa ajili ya
jina langu, wala hukuvunjika moyo.
4 Lakini ninayo hoja moja juu yako: wewe hunipendi tena
sasa kama pale awali.
5 Basi, pakumbuke pale ulipokuwa kabla ya kuanguka,
ukayaache madhambi yako, na kufanya kama ulivyofanya pale awali. La sivyo, naja
kwako na kukiondoa kinara chako mahali pake.
6 Lakini nakusifu juu ya kitu kimoja: wewe unayachukia
wanayoyatenda Wanikolai kama ninavyoyachukia mimi.
7 "Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho
anayoyaambia makanisa! "Wale wanaoshinda nitawapa haki ya kula matunda ya
mti wa uzima ulioko ndani ya bustani ya Mungu.
8 "Kwa malaika wa kanisa la Smurna andika hivi:
"Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye wa kwanza na wa mwisho, ambaye alikufa
na akaishi tena.
9 Najua taabu zako; najua pia umaskini wako, ingawaje kwa
kweli wewe ni tajiri; najua kashfa walizokufanyia wale wanaojiita Wayahudi
lakini si Wayahudi wa kweli, bali ni kundi lake Shetani.
10 Usiogope hata kidogo yale ambayo itakulazimu kuteseka.
Sikiliza! Ibilisi anataka kuwajaribu kwa kuwatia baadhi yenu gerezani; nanyi
mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Muwe waaminifu hata mpaka kufa, nami
nitawapeni taji ya uzima.
11 "Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho
anayoyaambia makanisa! "Wale wanaoshinda hawataumizwa na kifo cha pili.
12 "Kwa malaika wa kanisa la Pergamoni andika hivi:
"Huu ndio ujumbe wake yeye aliye na upanga mkali wenye kuwili.
13 Najua unakoishi: Wewe unaishi kwenye makao makuu ya
Shetani! Lakini bado unashikilia jina langu; hukuikana imani yako kwangu hata
siku zile Antipa shahidi wangu mwaminifu, alipouawa pale mahali anapoishi
Shetani.
14 Lakini ninayo machache dhidi yako: baadhi yenu ni
wafuasi wa Balaamu aliyemfundisha Balaki kuwatega wana wa Israeli wale vyakula
vilivyotambikiwa sanamu za kufanya uzinzi.
15 Vivyo hivyo, wako pia miongoni mwenu watu wanaofuata
mafundisho ya Wanikolai.
16 Basi, achana na madhambi yako. La sivyo, nitakuja kwako
upesi na kupigana na watu hao kwa upanga utokao kinywani mwangu.
17 "Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho
anayoyaambia makanisa! "Wale wanaoshinda nitawapa ile mana iliyofichika.
Nitawapa pia jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya ambalo hakuna mtu aliyelijua
isipokuwa tu wale wanaolipokea.
18 "Kwa malaika wa kanisa la Thuatira andika hivi:
"Huu ndio ujumbe wa Mwana wa Mungu, ambaye macho yake yametameta kama
moto, na miguu yake inang`aa kama shaba iliyosuguliwa.
19 Najua mambo yako yote. Najua upendo wako, imani yako,
utumishi wako na uvumilivu wako. Wewe unafanya vizuri zaidi sasa kuliko pale
awali.
20 Lakini nina hoja moja juu yako: wewe unamvumilia yule
mwanamke Yezabeli anayejiita nabii wa Mungu. Yeye huwafundisha na kuwapotosha
watumishi wangu wafanye uzinzi na kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu.
21 Nimempa muda wa kutubu dhambi zake, lakini hataki
kuachana na uzinzi wake.
22 Sikiliza! Sasa namtupa kitandani ambapo yeye pamoja na
wote waliofanya uzinzi naye watapatwa na mateso makali. Naam, nitafanya hivyo,
kama wasipotubu matendo yao mabaya waliyotenda naye.
23 Tena nitawaua wafuasi wake, ili makanisa yote yatambue
kwamba mimi ndiye ninayechunguza mioyo na fikira za watu.
24 "Lakini ninyi wengine mlioko huko Thuatira ambao
hamfuati mafundisho yake Yezabeli, na ambao hamkujifunza kile wanachokiita
`Siri ya Shetani`, nawaambieni kwamba sitawapeni mzigo mwingine.
25 Lazima mzingatie yale mliyo nayo sasa mpaka nitakapokuja.
26 "Wanaoshinda, na wale watakaozingatia mpaka mwisho
kutenda ninayotaka, nitawapa mamlaka juu ya mataifa. Naam, nitawapa uwezo
uleule nilioupokea kwa Baba: yaani, watayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma na
kuyavunjavunja kama chombo cha udongo. Tena nitawapa nyota ya asubuhi.
27 []
28 []
29 "Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho
anayoyaambia makanisa!
|