Chapter 3
1 "Kwa malaika wa kanisa la Sarde andika hivi:
"Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aliye na roho saba za Mungu na nyota
saba. Nayajua mambo yako yote; najua unajulikana kuwa na uhai kumbe umekufa!
2 Amka! Imarisha chochote chema kilichokubakia kabla nacho
hakijatoweka kabisa. Maana, mpaka sasa, sijayaona matendo yako kuwa ni
makamilifu mbele ya Mungu wangu.
3 Kumbuka, basi, yale uliyofundishwa na jinsi
ulivyoyasikia, uyatii na ubadili nia yako mbaya. Usipokesha nitakujia ghafla
kama mwizi, na wala hutaijua saa nitakapokujia.
4 Lakini wako wachache huko Sarde ambao hawakuyachafua
mavazi yao. Hao wanastahili kutembea pamoja nami wakiwa wamevaa mavazi meupe.
5 "Wale wanaoshinda, watavikwa mavazi meupe kama hao.
Nami sitayafuta majina yao kutoka katika kitabu cha uzima; tena nitawakiri
kwamba ni wangu mbele ya Baba yangu na mbele ya malaika wake.
6 "Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho
anayoyaambia makanisa!
7 "Kwa malaika wa kanisa la Filadelfia andika hivi:
"Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aliye mtakatifu na wa kweli, ambaye
anao ule ufunguo wa Daudi, na ambaye hufungua na hakuna mtu awezaye kufungua.
8 Nayajua mambo yako yote! Sasa, nimefungua mbele yako
mlango ambao hakuna mtu awezaye kuufunga; najua kwamba ingawa huna nguvu sana,
hata hivyo, umezishika amri zangu, umelitii neno langu wala hukulikana jina
langu.
9 Sikiliza! Nitawapeleka kwako watu wa kundi lake Shetani,
watu ambao hujisema kuwa ni Wayahudi, kumbe ni wadanganyifu. Naam, nitawapeleka
kwako na kuwafanya wapige magoti mbele yako wapate kujua kwamba kweli nakupenda
wewe.
10 Kwa kuwa wewe umezingatia agizo langu la kuwa na
uvumilivu, nami pia nitakutegemeza salama wakati ule wa dhiki inayoujia
ulimwengu mzima kuwajaribu wote wanaoishi duniani.
11 Naja kwako upesi! Linda, basi, ulicho nacho sasa, ili
usije ukanyang`anywa na mtu yeyote taji yako ya ushindi.
12 "Wale wanaoshinda nitawafanya wawe minara katika
Hekalu la Mungu wangu, na hawatatoka humo kamwe. Pia nitaandika juu yao jina la
Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu, yaani Yerusalemu mpya, mji ambao utashuka
kutoka juu mbinguni kwa Mungu wangu. Tena nitaandika juu yao jina langu jipya.
13 "Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho
anayoyaambia makanisa!
14 "Kwa malaika wa kanisa la Laodikea andika hivi:
"Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aitwaye `Amina`. Yeye ni shahidi
mwaminifu na wa kweli, ambaye ni chanzo cha viumbe vyote alivyoumba Mungu.
15 Nayajua mambo yako yote! Najua kwamba wewe si baridi
wala si moto. Afadhali ungekuwa kimojawapo: baridi au moto.
16 Basi, kwa kuwa hali yako ni vuguvugu, si baridi wala si
moto, nitakutapika!
17 Wewe unajisema, `Mimi ni tajiri; ninajitosheleza, sina
haja ya kitu chochote.` Kumbe, hujui kwamba wewe ni mnyonge, unahitaji kuhurumiwa,
maskini, kipofu tena uko uchi!
18 Nakushauri ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto
upate kuwa tajiri kweli. Tena afadhali ununue pia vazi jeupe, uvae na kufunika
aibu ya uchi wako. Nunua pia mafuta ukapake machoni pako upate kuona.
19 Mimi ndiye mwenye kumwonya na kumrudi yeyote
ninayempenda. Kwa hiyo kaza
moyo, achana na dhambi zako.
20
Sikiliza! Mimi nasimama mlangoni na kubisha hodi. Mtu akisikia sauti
yangu na kufungua mlango, nitaingia nyumbani kwake na kula chakula pamoja naye,
naye atakula pamoja nami.
21 "Wale wanaoshinda nitawaketisha pamoja nami juu ya
kiti changu cha enzi, kama vile mimi mwenyewe nilivyoshinda nikaketi pamoja na
Baba yangu juu ya kiti chake cha enzi.
22 "Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho
anayoyaambia makanisa!"
|