Chapter 4
1 Baada ya hayo nilitazama nikaona mlango umefunguliwa
mbinguni. Na ile sauti niliyoisikia pale awali ambayo ilikuwa kama sauti ya
tarumbeta, ikasema, "Njoo hapa juu nami nitakuonyesha mambo yatakayotukia
baadaye."
2 Mara
nikachukuliwa na Roho. Kumbe, huko mbinguni kuna kiti cha enzi na juu yake
ameketi mmoja.
3 Huyo
aliyeketi juu yake alikuwa kama almasi na jiwe zuri jekundu. Upinde wa mvua
ulikuwa unang`aa kama zumaridi na ulikizunguka kiti cha enzi pande zote.
4 Kulikuwa
na duara la viti ishirini na vinne kukizunguka kiti cha enzi, na juu ya viti
hivyo wazee ishirini na wanne walikuwa wameketi wamevaa mavazi meupe na taji za
dhahabu vichwani.
5 Umeme,
sauti na ngurumo, vilikuwa vinatoka kwenye hicho kiti cha enzi. Taa saba za
moto zilikuwa zinawaka mbele ya hicho kiti cha enzi. Taa hizo ni roho saba za
Mungu.
6 Mbele ya
kiti cha enzi kulikuwa na kitu kama bahari ya kioo, angavu kama jiwe linga`aalo
sana. Katika pande zote za hicho kiti cha enzi na kukizunguka, kilikuwa na
viumbe hai vinne. Viumbe hivyo vilikuwa vimejaa macho mbele na nyuma.
7 Kiumbe
cha kwanza kulikuwa kama simba, cha pili kama ng`ombe, cha tatu kilikuwa na
sura kama mtu, na cha nne kilikuwa kama tai anayeruka.
8 Viumbe
hivyo vinne vilikuwa na mabawa sita kila kimoja, na vilikuwa vimejaa macho,
ndani na nje. Usiku na mchana, bila kupumzika huimba: "Mtakatifu,
mtakatifu, mtakatifu ni Bwana, Mungu Mwenye Uwezo, aliyekuwako, aliyeko na
anayekuja!"
9 Kila
mara viumbe vinne vilipoimba nyimbo za kumtukuza, kumheshimu na kumshukuru huyo
aliyeketi juu ya kiti cha enzi, ambaye anaishi milele na milele,
10 wale
wazee ishirini na wanne hujiangusha mbele ya huyo aliyeketi juu ya kiti cha
enzi na kumwabudu huyo ambaye anaishi milele na milele; na huziweka taji zao
mbele ya kiti cha enzi wakisema:
11
"Wewe ni Bwana na Mungu wetu, unastahili utukufu na heshima na nguvu;
maana wewe uliumba vitu vyote, na kwa matakwa yako kila kitu kimepewa uhai na
uzima."
|