Chapter 5
1 Kisha
katika mkono wa kulia wa huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi, nikaona kitabu;
nacho kilikuwa kimeandikwa ndani na nje na kufungwa na mihuri saba.
2 Tena
nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kubwa: "Nani
anayestahili kuvunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu hicho?"
3 Lakini
hakupatikana mtu yeyote mbinguni, wala duniani, wala chini Kuzimu, aliyeweza
kukifungua hicho kitabu au kukitazama ndani.
4 Basi,
mimi nikalia sana kwa sababu hakupatikana mtu aliyestahili kukifungua, au
kukitazama ndani.
5 Kisha
mmoja wa wale wazee akaniambia, "Usilie! Tazama! Simba wa kabila la Yuda,
mjukuu maarufu wa Daudi, ameshinda. Yeye anaweza kuivunja mihuri yake saba na
kukifungua hicho kitabu."
6 Kisha
nikaona pale katikati ya kiti cha enzi Mwana kondoo amesimama, akizungukwa kila
upande na vile viumbe hai vinne, na wale wazee. Huyo Mwanakondoo alionekana
kana kwamba amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba ambayo ni roho saba
za Mungu zilizokuwa zimepelekwa kila mahali duniani.
7
Mwanakondoo akaenda, akakitwaa hicho kitabu kutoka mkono wa kulia wa yule aliyeketi
juu ya kiti cha enzi.
8 Mara tu
alipokwisha twaa hicho kitabu, vile viumbe hai vinne pamoja na wale wazee
ishirini na wanne walianguka kifudifudi mbele ya Mwanakondoo. Kila mmoja,
alikuwa na kinubi na bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni sala za watu
wa Mungu.
9 Basi,
wakaimba wimbo huu mpya: "Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu na
kuivunja mihuri yake. Kwa sababu wewe umechinjwa, na kwa damu yako umemnunulia
Mungu watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.
10 Wewe
umewafanya wawe ufalme wa makuhani wamtumikie Mungu wetu nao watatawala
duniani."
11 Kisha
nikatazama, nikasikia sauti ya malaika wengi sana, idadi isiyohesabika, maelfu
na maelfu. Walikuwa wamekaa kuzunguka kiti cha enzi, vile viumbe hai vinne na
wale wazee;
12
wakasema kwa sauti kuu: "Mwanakondoo aliyechinjwa anastahili kupokea
uwezo, utajiri, hekima, nguvu, utukufu na sifa."
13
Nikasikia viumbe vyote mbinguni, duniani, chini kuzimuni na baharini - viumbe
vyote ulimwenguni - vikisema: "Kwake yeye aketiye katika kiti cha enzi, na
kwa Mwanakondoo, iwe sifa na heshima na utukufu na enzi milele na milele."
14 Na vile viumbe vinne hai vikasema, "Amina!" Na
wale wazee wakaanguka kifudifudi, wakaabudu.
|