Chapter 6
1 Kisha nikamwona Mwanakondoo anavunja mhuri mmojawapo wa
ile mihuri saba. Nikasikia kimoja cha vile viumbe hai vinne kikisema kwa sauti
kama ya ngurumo, "Njoo!"
2 Mimi nikatazama, na kumbe palikuwa na farasi mmoja mweupe
hapo. Na mpanda farasi wake
alikuwa na upinde, akapewa na taji. Basi, akatoka kama mshindi aendelee
kushinda.
3 Kisha,
Mwanakondoo akavunja mhuri wa pili. Nikamsikia yule kiumbe hai wa pili akisema,
"Njoo!"
4 Nami
nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mwingine hapo, mwekundu. Mpanda farasi
wake alikabidhiwa jukumu la kuondoa amani duniani, watu wauane, akapewa upanga
mkubwa.
5 Kisha
Mwanakondoo akavunja mhuri wa tatu. Nikamsikia yule kiumbe hai wa tatu akisema,
"Njoo!" Nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mmoja hapo, mweusi.
Mpanda farasi wake alikuwa na vipimo viwili vya kupimia uzito mkononi mwake.
6
Nikasikia kitu kama sauti itokayo kwa vile viumbe hai vinne. Nayo ilisema,
"Kibaba kimoja cha unga wa ngano wa kiasi cha fedha dinari moja, na vibaba
vitatu vya shayiri kwa dinari moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!"
7 Kisha
Mwanakondoo akavunja mhuri wa nne. Nikamsikia yule kiumbe hai wa nne akisema,
"Njoo!"
8 Nami
nikatazama, na kumbe alikuwapo farasi mmoja hapo, rangi yake kijivu. Na jina la
mpanda farasi wake lilikuwa kifo, na Kuzimu alimfuata nyuma. Hao walipewa
mamlaka juu ya robo moja ya dunia, wawaue watu kwa upanga, njaa, tauni na kwa
wanyama wakali wa dunia.
9 Kisha
Mwanakondoo akavunja mhuri wa tano. Nikaona pale chini ya madhabahu ya
kufukizia ubani roho za wale waliouawa kwa sababu ya ujumbe wa Mungu, na kwa
sababu ya ushuhuda waliotoa.
10 Basi,
wakalia kwa sauti kubwa: "Ee Bwana, uliye mtakatifu na mwaminifu, mpaka
lini utakawia kulipiza kisasi kwa wakazi wote wa dunia kwa ajili ya kuuawa
kwetu?"
11
Wakapewa kila mmoja vazi refu jeupe, wakaambiwa wazidi kusubiri kwa muda mfupi,
mpaka itakapotimia idadi ya watumishi wenzao na ndugu ambao watawaua kama wao
wenyewe walivyouawa.
12 Kisha
nikatazama, na wakati Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa sita, kukawa na tetemeko
kubwa la ardhi; jua likawa jeusi kama gunia; mwezi wote ukawa mwekundu kama
damu;
13 nazo
nyota za mbingu zikaanguka juu ya ardhi kama matunda ya mtini yasiyokomaa
yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali.
14 Anga
likatoweka kama vile karatasi inavyokunjwakunjwa; milima yote na visima vyote
vikaondolewa mahali pake.
15 Kisha
wafalme wa duniani, wakuu, majemadari, matajiri, wenye nguvu, kila mtumwa na
mtu huru, wakajificha mapangoni na kwenye majabali milimani.
16
Wakaiambia hiyo milima na hayo majabali, "Tuangukieni, mkatufiche mbali na
yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na mbali na ghadhabu ya Mwanakondoo!
17 Maana
siku maalum ya ghadhabu yao imefika. Nani awezaye kuikabili?"
|