Chapter 8
1 Na Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa saba, kukawa kimya
mbinguni kwa muda wa nusu saa.
2 Kisha nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele ya
Mungu wamepewa tarumbeta saba.
3 Malaika mwingine akafika, akiwa anachukua chetezo cha
dhahabu, akasimama mbele ya madhabahu ya kufukizia ubani. Naye akapewa ubani
mwingi autoe sadaka pamoja na sala za watu wote wa Mungu, juu ya madhabahu ya
dhahabu iliyo mbele ya kiti cha enzi.
4 Moshi wa ubani ukapanda juu, pamoja na sala za watu wa
Mungu, kutoka mikononi mwake huyo malaika aliyekuwa mbele ya Mungu.
5 Kisha malaika akakichukua hicho chetezo, akakijaza moto
wa madhabahuni akakitupa duniani. Kukawa na ngurumo, sauti, umeme na tetemeko
la ardhi.
6 Kisha wale malaika saba wenye tarumbeta saba wakajiweka
tayari kupiga mbiu ya mgambo. ic
7 Malaika wa kwanza akapiga tarumbeta yake. Mchanganyiko wa
mvua ya mawe na moto, pamoja na damu, ukamwagwa juu ya nchi. Theluthi moja ya
nchi ikaungua, theluthi moja ya miti ikaungua, na majani yote mabichi
yakaungua.
8 Malaika wa pili akapiga tarumbeta yake. Na kitu kama
mlima mkubwa unaowaka moto ukatupwa baharini. Theluthi moja ya bahari ikawa
damu,
9 theluthi moja ya viumbe vya baharini vikafa na theluthi
moja ya meli zikaharibiwa.
10 Kisha malaika wa tatu akapiga tarumbeta yake. Na nyota
kubwa ikiwaka kama bonge la moto, ikaanguka kutoka mbinguni, na kutua juu ya
theluthi moja ya mito na chemchemi za maji.
11 (Nyota hiyo inaitwa "Uchungu.") Basi, theluthi
moja ya maji yakawa machungu; watu wengi wakafa kutokana na maji hayo, kwa
sababu yaligeuka kuwa machungu.
12 Kisha malaika wa nne akapiga tarumbeta yake. Ndipo
theluthi moja ya jua, ya mwezi na ya nyota ikapata pigo; hata mwangaza
ukapoteza theluthi moja ya mng`ao wake. Theluthi moja ya mchana ikakosa mwanga,
hali kadhalika na theluthi moja ya usiku.
13 Kisha nikatazama, nikasikia tai akiruka juu kabisa
angani anasema kwa sauti kubwa, "Ole, ole, ole kwa wanaoishi duniani
wakati malaika watatu waliobaki watakapopiga tarumbeta zao!"
|