Chapter 9
1 Kisha malaika wa tano akapiga tarumbeta yake. Nami
nikaona nyota iliyokuwa imeanguka juu ya nchi kutoka mbinguni. Nayo ikapewa
ufunguo wa shimo la Kuzimu.
2 Basi, nyota hiyo ikafungua shimo la Kuzimu, kukatoka
moshi wa tanuru kubwa. Jua na anga vikatiwa giza kwa moshi huo wa Kuzimu.
3 Nzige wakatoka katika moshi huo, wakaingia duniani
wakapewa nguvu kama ya ng`e.
4 Wakaamrishwa wasiharibu nyasi za nchi wala majani wala miti
yoyote, bali wawaharibu wale tu ambao hawakupigwa mhuri wa Mungu katika paji la
uso.
5 Nzige hao hawakuruhusiwa kuwaua watu, ila kuwatesa tu kwa
muda wa miezi mitano. Maumivu watakayosababisha ni kama maumivu yanayompata mtu
wakati anapoumwa na ng`e.
6 Muda huo watu watatafuta kifo lakini hawatakipata;
watatamani kufa lakini kifo kitawakimbia.
7 Kwa kuonekana, nzige hao walikuwa kama farasi waliowekwa
tayari kwa vita. Juu ya vichwa vyao walikuwa na taji zilizo kama za dhahabu, na
nyuso zao zilikuwa kama za binadamu.
8 Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake, na meno yao
yalikuwa kama meno ya simba.
9 Vifua vyao vilikuwa vimefunikwa kitu kama ngao ya chuma.
Sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya msafara wa magari ya farasi wengi
wanaokimbilia vitani.
10 Walikuwa na mikia na miiba kama ng`e, na kwa mikia hiyo,
walikuwa na nguvu ya kuwadhuru watu kwa muda wa miezi mitano.
11 Tena wanaye mfalme anayewatawala, naye ndiye malaika wa
kuzimu; jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kigiriki ni Apolioni, yaani
mwangamizi.
12 Maafa ya kwanza yamepita; bado mengine mawili yanafuata.
13 Kisha malaika wa sita akapiga tarumbeta yake. Nami
nikasikia sauti moja kutoka katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyokuwa
mbele ya Mungu.
14 Sauti hiyo ikamwambia huyo malaika wa sita mwenye
tarumbeta, "Wafungulie malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa
`Eufrate!"`
15 Naye akawafungulia malaika hao wanne ambao walikuwa
wametayarishwa kwa ajili ya saa hiyo ya siku ya mwezi huo, wa mwaka huohuo,
kuua theluthi moja ya wanaadamu.
16 Nilisikia idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa
milioni mia mbili.
17 Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi
katika hiyo njozi: Walikuwa na ngao vifuani zilizokuwa moto mtupu, zenye rangi
ya samawati na njano kama kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vya
simba; na moto, moshi, na kiberiti vilikuwa vinatoka kinywani mwao.
18 Theluthi moja ya wanaadamu waliuawa kwa mabaa hayo
matatu yaani, moto, moshi na kiberiti, yaliyokuwa yanatoka katika vinywa vyao;
19 maana nguvu ya farasi hao ilikuwa vinywani mwao na
katika mikia yao. Mikia yao ilikuwa na vichwa kama nyoka, na waliitumia hiyo
kuwadhuru watu.
20 Wanaadamu wengine waliobaki ambao hawakuuawa na mabaa
hayo, hawakugeuka na kuviacha vitu walivyokuwa wametengeneza kwa mikono yao
wenyewe; bali wakaendelea kuabudu pepo, sanamu za dhahabu, fedha, shaba, mawe
na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, kusikia wala kutembea.
21 Wala hawakutubu na kuacha kufanya mauaji, uchawi,
uzinzi, na wizi.
|