Chapter 10
1 Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka
kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu, na upinde wa mvua kichwani mwake. Uso
wake ulikuwa kama jua, na miguu yake ilikuwa kama moto.
2 Mikononi mwake alishika kitabu kidogo kimefunguliwa.
Aliweka mguu wake wa kulia juu ya bahari, na wa kushoto juu ya nchi kavu,
3 na kuita kwa sauti kubwa kama ya mngurumo wa simba.
Alipopaaza sauti, ngurumo saba ziliitikia kwa kishindo.
4 Na hizo ngurumo saba ziliposema, mimi nikataka kuandika.
Lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni: "Maneno ya ngurumo hizo saba ni
siri; usiyaandike!"
5 Kisha yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na
juu ya nchi kavu akainua mkono wake wa kulia juu mbinguni,
6 akaapa kwa jina la Mungu aishiye milele na milele, Mungu
aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo, dunia na vyote
vilivyomo. Akasema, "Wakati wa kusubiri zaidi umekwisha!
7 Lakini wakati ule malaika wa saba atakapotoa sauti yake,
wakati atakapopiga tarumbeta yake, Mungu atakamilisha mpango wake wa siri kama
alivyowatangazia watumishi wake manabii."
8 Kisha ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni
pale awali ikasema nami tena: "Nenda ukakichukue kile kitabu
kilichofunguliwa, kilicho mkononi mwa malaika asimamaye juu ya bahari na juu ya
nchi kavu."
9 Basi, nikamwendea huyo malaika, nikamwambia anipe hicho
kitabu kidogo. Naye akaniambia, "Kichukue, ukile; kinywani mwako kitakuwa
kitamu kama asali, lakini tumboni kitakuwa kichungu!"
10 Basi, nikakichukua kitabu hicho kidogo kutoka mkononi
mwa huyo malaika, nikakila; nacho kilikuwa kitamu kinywani mwangu kama asali,
lakini nilipokimeza kikawa kichungu tumboni mwangu.
11 Kisha nikaambiwa, "Inakubidi tena kutangaza ujumbe
wa Mungu kuhusu watu wengi, mataifa, watu wa lugha nyingi na wafalme!"
|