Chapter 11
1 Kisha nikapewa mwanzi uliokuwa kama kijiti cha kupimia,
nikaambiwa, "Inuka, ukalipime Hekalu la Mungu, madhabahu ya kufukizia
ubani, na ukawahesabu watu wanaoabudu ndani ya Hekalu.
2 Lakini uache ukumbi ulio nje ya Hekalu; usiupime, maana
huo umekabidhiwa watu wa mataifa mengine, ambao wataukanyanga mji Mtakatifu kwa
muda wa miezi arobaini na miwili.
3 Nami nitawatuma mashahidi wangu wawili ili watangaze ujumbe
wa Mungu kwa muda huo wa siku elfu moja mia mbili na sitini wakiwa wamevaa
mavazi ya magunia."
4 Hao mashahidi wawili ni miti miwili ya Mizeituni na taa
mbili zinazosimama mbele ya Bwana wa dunia.
5 Kama mtu akijaribu kuwadhuru, moto hutoka kinywani mwao
na kuwaangamiza adui zao; na kila mtu atakayejaribu kuwadhuru atakufa namna
hiyo.
6 Hao wanayo mamlaka ya kufunga anga, mvua isinyeshe wakati
wanapotangaza ujumbe wa Mungu. Tena wanayo mamlaka ya kuzigeuza chemchemi zote
za maji ziwe damu, na ya kusababisha maafa ya kila namna duniani kila mara
wapendavyo.
7 Lakini wakisha maliza kutangaza ujumbe huo, mnyama
atokaye shimoni kuzimu atapigana nao, atawashinda na kuwaua.
8 Maiti zao zitabaki katika barabara za mji mkuu ambapo
Bwana wao alisulubiwa; jina la kupanga la mji huo ni Sodoma au Misri.
9 Watu wa kila kabila, lugha, taifa na rangi wataziangalia
maiti hizo kwa muda wa siku tatu na nusu, na hawataruhusu zizikwe.
10 Watu waishio duniani watafurahia kifo cha hao wawili.
Watafanya sherehe na kupelekeana zawadi maana manabii hawa wawili walikuwa
wamewasumbua mno watu wa dunia.
11 Lakini baada ya zile siku tatu na nusu pumzi ya uhai
kutoka kwa Mungu iliwaingia, nao wakasimama; wote waliowaona wakaingiwa na hofu
kuu.
12 Kisha hao manabii wawili wakasikia sauti kubwa kutoka
mbinguni ikiwaambia, "Njoni hapa juu!" Nao wakapanda juu mbinguni katika
wingu, maadui wao wakiwa wanawatazama.
13 Wakati huohuo, kukatokea tetemeko kubwa la ardhi, sehemu
moja ya kumi ya ardhi ikaharibiwa. Watu elfu saba wakauawa kwa tetemeko hilo la
ardhi. Watu waliosalia wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni.
14 Maafa ya pili yamepita; lakini tazama! Maafa ya tatu
yanafuata hima.
15 Kisha malaika wa saba akapiga tarumbeta yake. Na sauti
kuu zikasikika mbinguni zikisema, "Sasa utawala juu ya ulimwengu ni wa
Bwana wetu na Kristo wake. Naye atatawala milele na milele!"
16 Kisha wale wazee ishirini na wanne walioketi mbele ya
Mungu katika viti vyao vya enzi, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu,
17 wakisema: "Bwana Mungu Mwenye uwezo, uliyeko na
uliyekuwako! Tunakushukuru, maana umetumia nguvu yako kuu ukaanza kutawala!
18 Watu wa mataifa waliwaka hasira, maana wakati wa
ghadhabu yako umefika, wakati wa kuwahukumu wafu. Ndio wakati wa kuwatuza
watumishi wako manabii, watu wako na wote wanaolitukuza jina lako, wakubwa kwa
wadogo. Ni wakati wa kuwaangamiza wale wanaoangamiza dunia."
19 Hekalu la Mungu mbinguni likafunguliwa, na Sanduku la
Agano lake likaonekana Hekaluni mwake. Kisha kukatokea umeme, sauti, ngurumo,
tetemeko la ardhi, na mvua kubwa ya mawe.
|