Chapter 13
1 Kisha nikaona mnyama mmoja akitoka baharini. Alikuwa na vichwa saba na pembe
kumi, na kila pembe ilikuwa na taji. Jina la kashfa lilikuwa limeandikwa juu ya
vichwa hivyo.
2 Mnyama
huyo niliyemwona alikuwa kama chui; miguu yake ilikuwa kama ya dubu, na kinywa
chake kama cha simba. Lile joka likampa huyo mnyama nguvu yake, kiti chake cha
enzi na uwezo mkuu.
3 Kichwa
kimojawapo cha huyo mnyama kilionekana kama kilikwisha jeruhiwa vibaya sana,
lakini jeraha hilo lilikuwa limepona. Dunia nzima ilishangazwa na huyo mnyama
na kumfuata.
4 Watu
wote wakaliabudu lile joka kwa sababu lilimpa huyo mnyama uwezo wake.
Wakamwabudu pia huyo mnyama wakisema, "Nani aliye kama huyu mnyama? Ni
nani awezaye kupigana naye?"
5 Kisha
huyo mnyama akaruhusiwa kusema maneno ya kujigamba na kumkufuru Mungu;
akaruhusiwa kuwa na mamlaka kwa muda wa miezi arobaini na miwili.
6 Basi,
akaanza kumtukana Mungu, kulitukana jina lake, makao yake, na wote wakaao
mbinguni.
7
Aliruhusiwa kuwapiga vita na kuwashinda watu wa Mungu. Alipewa mamlaka juu ya
watu wa kila kabila, ukoo, lugha na taifa.
8 Wote
waishio duniani watamwabudu isipokuwa tu wale ambao majina yao yameandikwa
tangu mwanzo wa ulimwengu katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo aliyechinjwa.
9
"Aliye na masikio, na asikie!
10
Waliokusudiwa kuchukuliwa mateka lazima watatekwa; waliokusudiwa kuuawa kwa
upanga lazima watauawa kwa upanga. Kutokana na hayo ni lazima watu wa Mungu
wawe na uvumilivu na imani."
11 Kisha
nikamwona mnyama mwingine anatoka ardhini. Alikuwa na pembe mbili kama pembe za
kondoo, na aliongea kama joka.
12 Alikuwa
na mamlaka kamili kutoka kwa yule mnyama wa kwanza, na akautumia uwezo huo
mbele ya huyo mnyama. Akailazimisha dunia yote na wote waliomo humo kumwabudu
huyo mnyama wa kwanza ambaye alikuwa na jeraha la kifo lililokuwa limepona.
13 Basi,
huyu mnyama wa pili akafanya miujiza mikubwa hata akasababisha moto kutoka
mbinguni ushuke duniani mbele ya watu.
14
Aliwapotosha wakazi wa dunia kwa miujiza hiyo aliyojaliwa kutenda mbele ya
mnyama wa kwanza. Aliwaambia wakazi wa dunia watengeneze sanamu kwa heshima ya
yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi tena.
15 Kisha
alijaliwa kuipulizia uhai hiyo sanamu ya yule mnyama wa kwanza, hata ikaweza
kuongea na kuwaua watu wote ambao hawakuiabudu.
16
Aliwalazimisha wote, wadogo na wakubwa, matajiri na maskini, watu huru na
watumwa, watiwe alama juu ya mikono yao ya kulia au juu ya paji za nyuso zao.
17 Akapiga
marufuku mtu yeyote kununua au kuuza kitu isipokuwa tu mtu aliyetiwa alama
hiyo, yaani jina la yule mnyama au tarakimu ya jina hilo.
18 Hapa ni lazima kutumia ujasiri! Mwenye akili anaweza
kufafanua maana ya tarakimu ya mnyama huyo, maana ni tarakimu yenye maana ya
mtu fulani. Tarakimu hiyo ni mia sita sitini na sita.
|