Chapter 14
1 Kisha nikaona mlima Sioni, na Mwanakondoo amesimama juu
yake; pamoja naye walikuwa watu mia moja arobaini na nne elfu ambao juu ya paji
za nyuso zao walikuwa wameandikwa jina la Mwanakondoo na jina la Baba yake.
2 Basi, nikasikia sauti kutoka mbinguni, sauti iliyokuwa
kama sauti ya maji mengi na kama sauti ya ngurumo kubwa. Sauti niliyosikia
ilikuwa kama sauti ya wachezaji muziki wakipiga vinubi vyao.
3 Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na
mbele ya wale viumbe hai wanne na wale wazee. Hakuna mtu aliyeweza kujifunza
wimbo huo isipokuwa hao watu mia moja arobaini na nne elfu waliokombolewa
duniani.
4 Watu hao ndio wale waliojiweka safi kwa kutoonana kimwili
na wanawake, nao ni mabikira. Wao humfuata Mwanakondoo kokote aendako.
Wamekombolewa kutoka miongoni mwa binadamu wengine, wakawa wa kwanza kutolewa
kwa Mungu na kwa Mwanakondoo.
5 Hawakupata kamwe kuwa waongo; hawana hatia yoyote.
6 Kisha nikamwona malaika mwingine anaruka juu angani akiwa
na Habari Njema ya milele ya Mungu, aitangaze kwa watu wote waishio duniani,
kwa mataifa yote, makabila yote, watu wa lugha zote na rangi zote.
7 Akasema kwa sauti kubwa, "Mcheni Mungu na kumtukuza!
Maana saa imefika ya kutoa hukumu yake. Mwabuduni yeye aliyeumba mbingu na
nchi, bahari na chemchemi za maji."
8 Malaika wa pili alimfuata huyo wa kwanza akisema,
"Ameanguka! Naam, Babuloni mkuu ameanguka! Babuloni ambaye aliwapa mataifa
yote wainywe divai yake - divai kali ya uzinzi wake!"
9 Na malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa
sauti kubwa, "Yeyote anayemwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali
kutiwa alama yake juu ya paji la uso wake au juu ya mkono wake,
10 yeye mwenyewe atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu,
ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchanganywa na maji.
Mtu huyo atateseka ndani ya moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na
mbele ya Mwanakondoo.
11 Moshi wa moto unaowatesa kupanda juu milele na milele.
Watu hao waliomwabudu huyo mnyama na sanamu yake, na kutiwa alama ya jina lake,
hawatakuwa na nafuu yoyote usiku na mchana."
12 Kutokana na hayo, ni lazima watu wa Mungu, yaani watu
wanaotii amri ya Mungu na kumwamini Yesu, wawe na uvumilivu.
13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema,
"Andika! Heri watu ambao tangu sasa wanakufa wakiwa wameungana na
Bwana." Naye Roho asema, "Naam! Watapumzika kutoka taabu zao; maana
matunda ya jasho lao yatawafuata."
14 Kisha nikatazama, na kumbe palikuwapo wingu jeupe hapo.
Na juu ya wingu hilo kulikuwa na kiumbe kama mtu. Alikuwa amevaa taji ya
dhahabu kichwani, na kushika mundu mkononi mwake.
15 Kisha malaika mwingine akatoka Hekaluni, na kwa sauti
kubwa akamwambia yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu, "Tafadhali, tumia
mundu wako ukavune mavuno, maana wakati wa mavuno umefika; mavuno ya dunia
yameiva."
16 Basi, yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akautupa mundu
wake duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa.
17 Kisha malaika mwingine akatoka katika Hekalu mbinguni
akiwa na mundu wenye makali.
18 Kisha malaika mwingine msimamizi wa moto, akatoka
madhabahuni akamwambia kwa sauti kubwa yule malaika mwenye mundu wenye makali,
"Nawe tia huo mundu wako mkali, ukakate vichala vya mizabibu ya dunia,
maana zabibu zake zimeiva!"
19 Basi, malaika huyo akautupa mundu wake duniani, akakata
zabibu za dunia, akazitia ndani ya chombo kikubwa cha kukamulia zabibu, chombo
cha ghadhabu ya Mungu.
20 Zabibu zikakamuliwa ndani ya hilo shinikizo lililoko nje
ya mji, na damu ikatoka katika shinikizo hilo mtiririko mrefu kiasi cha mita
mia tatu na kina chake kiasi cha mita mia mbili.
|