Chapter 15
1 Kisha nikaona ishara nyingine mbinguni, kubwa na ya
kushangaza. Palikuwa hapo malaika saba wenye mabaa makubwa saba ya mwisho. Kwa
mabaa hayo makubwa saba, ghadhabu ya Mungu imekamilishwa.
2 Kisha nikaona kitu kama bahari ya kioo, imechanganywa na
moto. Nikawaona pia wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake na ambaye
jina lake lilitajwa kwa ile tarakimu. Watu hao walikuwa wamesimama kando ya
hiyo bahari ya kioo, wakiwa na vinubi walivyopewa na Mungu.
3 Walikuwa wakiimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu, na
wimbo wa Mwanakondoo: "Bwana Mungu Mwenye Uwezo, matendo yako ni makuu
mno! Ewe Mfalme wa mataifa, njia zako ni za haki na za kweli!
4 Bwana, ni nani asiyekucha wewe? Nani asiyelitukuza jina
lako? Wewe peke yako ni Mtakatifu. Mataifa yote yatakujia na kukuabudu maana
matendo yako ya haki yameonekana na wote."
5 Baada ya hayo nikaona Hekalu limefunguliwa mbinguni, na
ndani yake hema ionyeshayo kuwapo kwa Mungu.
6 Basi, wale malaika saba wenye mabaa saba wakatoka humo
Hekaluni, wakiwa wamevaa nguo za kitani safi zenye kung`aa, na kanda za dhahabu
vifuani mwao.
7 Kisha, mmojawapo wa vile viumbe vinne akawapa hao malaika
saba mabakuli ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele.
8 Hekalu likajaa moshi uliosababishwa na utukufu na nguvu
ya Mungu, na hakuna mtu aliyeweza kuingia Hekaluni mpaka mwisho wa mabaa
makubwa saba ya wale malaika saba.
|