Chapter 16
1 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka Hekaluni ikiwaambia
wale malaika saba, "Nendeni mkamwage mabakuli hayo saba ya ghadhabu ya
Mungu duniani."
2 Basi, malaika wa kwanza akaenda akamwaga bakuli lake juu
ya nchi. Mara madonda mabaya na ya kuumiza sana yakawapata wote waliokuwa na
alama ya yule mnyama, na wale walioiabudu sanamu yake.
3 Kisha malaika wa pili akamwaga bakuli lake baharini. Nayo
bahari ikawa damu tupu kama damu ya mtu aliyekufa, na viumbe vyote hai baharini
vikafa.
4 Malaika wa tatu akamwaga bakuli lake katika mito na
chemchemi za maji, navyo vikageuka damu.
5 Nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema, "Ewe
mtakatifu, Uliyeko na uliyekuwako! Wewe ni mwenye haki katika hukumu hii
uliyotoa.
6 Maana waliimwaga damu ya watu wako na ya manabii, nawe
umewapa damu wainywe; wamestahili hivyo!"
7 Kisha nikasikia sauti madhabahuni ikisema, "Naam,
Bwana Mungu Mwenye Uwezo! Hukumu zako ni za kweli na haki!"
8 Kisha malaika wa nne akamwaga bakuli lake juu ya jua. Jua
likapewa nguvu ya kuwachoma watu kwa moto wake.
9 Basi, watu wakaunguzwa vibaya sana; wakamtukana Mungu
aliye na uwezo juu ya mabaa hayo makubwa. Lakini hawakuziacha dhambi zao na
kumtukuza Mungu.
10 Kisha malaika wa tano akamwaga bakuli lake juu ya makao
makuu ya yule mnyama. Giza likauvamia utawala wake, watu wakauma ndimi zao kwa
sababu za maumivu,
11 wakamtukana Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu yao
na madonda yao. Lakini hawakuyaacha matendo yao mabaya.
12 Kisha malaika wa sita akamwaga bakuli lake juu ya mto mkubwa
uitwao Eufrate. Maji yake yakakauka, na hivyo njia ilitengenezwa kwa ajili ya
wafalme wa mashariki.
13 Kisha nikaona pepo wabaya watatu walio kama vyura,
wakitoka kinywani mwa yule joka, kinywani mwa yule mnyama, na kinywani mwa yule
nabii wa uongo.
14 Hawa ndio roho za pepo wafanyao miujiza. Ndio
wanaokwenda kwa wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya pamoja kwa ajili ya
vita kuu Siku ile ya Mungu Mwenye Uwezo.
15 "Sikiliza! Mimi naja kama mwizi! Heri mtu akeshaye
na kuvaa nguo zake ili asije akaenda uchi huko na huko mbele ya watu."
16 Basi, roho hao wakawakusanya hao wafalme mahali paitwapo
kwa Kiebrania Harmagedoni.
17 Kisha malaika wa saba akamwaga bakuli lake hewani. Sauti
kubwa ikasikika kutoka kwenye kiti cha enzi, Hekaluni, ikisema, "Mwisho
umefika!"
18 Kukatokea umeme, kelele, ngurumo na tetemeko kubwa la
ardhi ambalo halijapata kutokea tangu Mungu alipomuumba mtu.
19 Mji ule mkuu ukapasuliwa sehemu tatu, nayo miji ya
mataifa ikateketea. Babuloni, mji mkuu, haukusahauliwa na Mungu. Aliunywesha
kikombe cha divai ya ghadhabu yake kuu.
20 Visiwa vyote vikatoweka, nayo milima haikuonekena tena.
21 Mvua ya mawe makubwa yenye uzito wa kama kilo hamsini
kila moja, ikawanyeshea watu. Nao wakamtukana Mungu kwa sababu ya mapigo ya
mvua hiyo ya mawe. Naam, pigo la mvua hiyo ya mawe lilikuwa kubwa mno.
|