Chapter 17
1 Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na bakuli akaja,
akaniambia, "Njoo, mimi nitakuonyesha adhabu aliyopewa yule mzinzi mkuu,
mji ule uliojengwa juu ya maji mengi.
2 Wafalme wa dunia wamefanya uzinzi pamoja naye; na wakazi
wa dunia wamelewa divai ya uzinzi wake."
3 Kisha, Roho akanikumba, akaniongoza mpaka jangwani. Huko
nikamwona mwanamke ameketi juu ya mnyama mwekundu. Mnyama huyo alikuwa
ameandikwa kila mahali majina ya makufuru; alikuwa na vichwa saba na pembe
kumi.
4 Mwanamke huyo alikuwa amevaa vazi la rangi ya zambarau na
nyekundu; alikuwa amejipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu. Mkononi
mwake alishika kikombe cha dhahabu ambacho kilikuwa kimejaa machukizo na mambo
machafu yanayoonyesha uzinzi wake.
5 Alikuwa ameandikwa juu ya paji la uso wake jina la fumbo
"Babuloni mkuu, mama wa wazinzi na wa mambo yote ya kuchukiza sana
duniani."
6 Nikamwona huyo mwanamke amelewa damu ya watu wa Mungu, na
damu ya watu waliouawa kwa sababu ya kumtangaza Yesu. Nilipomwona nilishangaa
mno.
7 Lakini malaika akaniambia, "Kwa nini unashangaa?
Mimi nitakuambia maana iliyofichika ya mwanamke huyu na mnyama huyo amchukuaye
ambaye ana vichwa saba na pembe kumi.
8 Huyo mnyama uliyemwona alikuwa hai hapo awali, lakini
sasa amekufa. Hata hivyo, karibu sana atapanda kutoka shimoni kuzimu, lakini
ataangamizwa. Wanaoishi duniani watashangaa; naam, watu wote ambao majina yao
hayakupata kuandikwa katika kitabu cha uzima tangu mwanzo wa ulimwengu,
watashangaa kumwona huyo mnyama ambaye hapo awali, aliishi, kisha akafa na sasa
anatokea tena!
9 "Hapa panahitaji akili na hekima! Hivyo vichwa saba
ni vilima saba, na huyo mwanamke anaketi juu yake. Vichwa hivyo pia ni wafalme
saba.
10 Kati ya hao wafalme saba, watano wamekwisha angamia,
mmoja anatawala bado, na yule mwingine bado hajafika; na atakapofika atabaki
kwa muda mfupi.
11 Huyo mnyama ambaye alikuwa anaishi hapo awali lakini
sasa haishi tena ni mfalme wa nane, naye pia ni miongoni mwa hao saba, na
anakwenda zake kuharibiwa.
12 "Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme ambao bado
hawajaanza kutawala. Lakini watapewa mamlaka ya kutawala kwa muda wa saa moja
pamoja na yule mnyama.
13 Shabaha ya hawa kumi ni moja, na watampa yule mnyama
nguvu na mamlaka yao yote.
14 Watapigana na Mwanakondoo, lakini Mwanakondoo pamoja na wale
aliowaita na kuwachagua, ambao ni waaminifu, atawashinda kwa sababu yeye ni
Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme."
15 Malaika akaniambia pia, "Yale maji uliyoyaona pale
alipokaa yule mzinzi, ni mataifa, watu wa kila rangi na lugha.
16 Pembe zile kumi ulizoziona na yule mnyama watamchukia
huyo mzinzi. Watachukua kila kitu alicho nacho na kumwacha uchi; watakula nyama
yake na kumteketeza kwa moto.
17 Maana Mungu ametia mioyoni mwao nia ya kutekeleza shabaha
yake, yaani kwa kukubaliana wao kwa wao na kumpa huyo mnyama mamlaka yao ya
kutawala, mpaka hapo neno la Mungu litakapotimia.
18 "Na yule mwanamke uliyemwona ndio ule mji mkuu
unaowatawala wafalme wa dunia."
|