Chapter 7
1
"Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu;
2 kwa maana
jinsi mnavyowahukumu wengine, ndivyo nanyi mtakavyohukumiwa; na kipimo kilekile
mnachotumia kwa wengine ndicho Mungu atakachotumia kwenu.
3 Kwa nini
wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti
iliyoko jichoni mwako?
4 Au, wawezaje
kumwambia ndugu yako, `Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako`, wakati
wewe mwenyewe unayo boriti jichoni mwako?
5 Mnafiki wewe!
Ondoa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako na hapo ndipo utaona waziwazi kiasi
cha kuweza kuondoa kibanzi kilichoko jichoni mwa ndugu yako.
6 "Msiwape
mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua ninyi; wala msiwatupie
nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga.
7 "Ombeni,
nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni, nanyi mtafunguliwa.
8 Maana, aombaye
hupewa, atafutaye hupata, na abishaye hufunguliwa.
9 Je, kuna
yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe?
10 Au je,
akimwomba samaki, atampa nyoka?
11 Kama basi
ninyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu
wa mbinguni atafanya zaidi: atawapa mema wale wanaomwomba.
12
"Watendeeni wengine yale mnayotaka wao wawatendee ninyi. Hii ndiyo maana
ya Sheria ya Mose na mafundisho ya manabii.
13
"Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye
maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni
wengi.
14 Lakini
njia inayoongoza kwenye uzima ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni
mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo.
15
"Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni
mbwa mwitu wakali.
16
Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au
tini katika mbigili? La!
17 Basi,
mti mwema huzaa matunda mema, na mti mbaya huzaa matunda mabaya.
18 Mti
mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mema.
19 Kila
mti usiozaa matunda mema utakatwa na kutupwa motoni.
20 Kwa
hiyo, mtawatambua kwa matendo yao. ic
21
"Si kila aniambiaye, `Bwana, Bwana,` ataingia katika Ufalme wa mbinguni;
ila ni yule tu anayetimiza mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
22 Wengi
wataniambia Siku ile ya hukumu: `Bwana, Bwana! kwa jina lako tulitangaza ujumbe
wako, na kwa jina lako tuliwatoa pepo na kufanya miujiza mingi.`
23 Hapo
nitawaambia: `Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni mbele yangu, enyi watenda maovu.`
24
"Kwa sababu hiyo, kila mtu anayeyasikia maneno yangu na kuyazingatia,
anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba.
25 Mvua
ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini
haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba.
26
"Lakini yeyote anayesikia maneno yangu haya bila kuyazingatia, anafanana
na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga.
27 Mvua
ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo, nayo
ikaanguka; tena kwa kishindo kikubwa."
28 Yesu
alipomaliza kusema maneno hayo, umati wa watu ukashangazwa na mafundisho yake.
29 Hakuwa
kama walimu wao wa Sheria, bali alifundisha kwa mamlaka.
|