Chapter 18
1 Baada ya hayo, nilimwona malaika mwingine akishuka kutoka
mbinguni. Alikuwa na uwezo
mkuu, na dunia ikamulikwa na mng`ao wake.
2 Basi,
akapaaza sauti kwa nguvu akisema, "Umeanguka; Babuloni mkuu umeanguka!
Sasa umekuwa makao ya mashetani na pepo wachafu; umekuwa makao ya ndege wachafu
na wa kuchukiza mno.
3 Maana
mataifa yote yalileweshwa kwa divai kali ya uzinzi wake, nao wafalme wa dunia
wamefanya uzinzi naye. Nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na
anasa zake zisizo na kipimo."
4 Kisha
nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema, "Watu wangu, ondokeni
kwake, ili msishirikiane naye katika dhambi zake, msije mkaipata adhabu yake.
5 Kwa
maana dhambi zake zimekuwa nyingi mno, zimelundikana mpaka mbinguni, na Mungu
ameyakumbuka maovu yake.
6
Mtendeeni kama alivyowatendea ninyi; mlipeni mara mbili kwa yale aliyoyatenda.
Jazeni kikombe chake kwa kinywaji kikali mara mbili zaidi ya kile alichowapeni.
7 Mpeni
mateso na uchungu kadiri ya kujigamba kwake, na kuishi kwake kwa anasa. Maana
anajisemea moyoni: `Ninaketi hapa; mimi ni malkia. Mimi si mjane, wala
sitapatwa na uchungu!`
8 Kwa
sababu hiyo mabaa yake yatampata kwa siku moja: ugonjwa, huzuni na njaa.
Atachomwa moto, maana Bwana Mungu mwenye kumhukumu ni Mwenye Uwezo."
9 Wafalme
wa Dunia waliofanya uzinzi naye na kuishi naye maisha ya anasa wataomboleza na
kulia wakati watakapoona moshi wa mji huo unaoteketea.
10
Wanasimama kwa mbali kwa sababu ya kuogopa mateso yake, na kusema, "Ole!
Ole kwako Babuloni, mji maarufu na wenye nguvu! Kwa muda wa saa moja tu adhabu
yako imekupata."
11
Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumfanyia matanga, maana hakuna mtu
anayenunua tena bidhaa zao;
12 hakuna
tena wa kununua dhahabu yao, fedha, mawe ya thamani na lulu, kitani na nguo za
rangi ya zambarau, hariri na nguo nyekundu; vyombo vya kila aina ya miti ya
pekee, vyombo vya pembe za ndovu, vya miti ya thamani kubwa, vya shaba, chuma
na marmari;
13
mdalasini, viungo, ubani, manemane, udi, divai, mafuta, unga na ngano, ng`ombe
na kondoo, farasi na magari ya kukokotwa, watumwa wao na hata maisha ya watu.
14
Wafanyabiashara wanamwambia: "Faida yote uliyotazamia imetoweka, na
utajiri na fahari vimekuponyoka; hutaweza kuvipata tena!"
15 Wafanya
biashara waliotajirika kutokana na mji huo, watasimama mbali kwa sababu ya hofu
ya mateso yake, watalalamika na kuomboleza,
16
wakisema, "Ole! Ole kwa mji huu mkuu. Ulizoea kuvalia nguo za kitani, za
rangi ya zambarau na nyekundu, na kujipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na
lulu!
17 Kwa saa
moja tu utajiri wako umetoweka!" Halafu manahodha wote na wasafiri wao,
wanamaji na wote wanaofanya kazi baharini, walisimama kwa mbali,
18 na
walipouona moshi wa moto ule uliouteketeza, wakalia kwa sauti: "Hakujapata
kuwako mji kama mji huu mkuu!"
19
Wakajimwagia vumbi juu ya vichwa vyao wakilia kwa sauti na kuomboleza:
"Ole! Ole kwako mji mkuu! Ni mji ambamo wote wenye meli zisafirizo
baharini walitajirika kutokana na utajiri wake. Kwa muda wa saa moja tu
umepoteza kila kitu!"
20 Furahi
ee mbingu, kwa sababu ya uharibifu wake. Furahini watu wa Mungu, mitume na
manabii! Kwa maana Mungu ameuhukumu kwa sababu ya mambo uliyowatenda ninyi!
21 Kisha
malaika mmoja mwenye nguvu sana akainua jiwe mfano wa jiwe kubwa la kusagia,
akalitupa baharini akisema, "Ndivyo, Babuloni atakavyotupwa na kupotea
kabisa.
22 Sauti
za vinubi za muziki, sauti za wapiga filimbi na tarumbeta hazitasikika tena
ndani yako. Hakuna fundi wa namna yoyote ile atakayepatikana tena ndani yako;
wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikika tena ndani yako.
23 Mwanga
wa taa hautaonekana tena ndani yako; sauti za bwana arusi na bibi arusi
hazitasikika tena ndani yako. Wafanyabiashara wako walikuwa wakuu duniani, na
kwa uchawi wako mataifa yote yalipotoshwa!"
24 Mji huo
uliadhibiwa kwani humo mlipatikana damu ya manabii, damu ya watu wa Mungu na
damu ya watu wote waliouawa duniani.
|