Chapter 19
1 Baada ya
hayo nikasikia kitu kama sauti kubwa ya umati wa watu wengi mbinguni ikisema,
"Haleluya! Ukombozi, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!
2 Maana
hukumu yake ni ya kweli na ya haki. Amemhukumu yule mzinzi mkuu ambaye alikuwa
ameipotosha dunia kwa uzinzi wake. Amemwadhibu kwa sababu ya kumwaga damu ya
watumishi wake!"
3
Wakasema, "Asifiwe Mungu! Moshi wa moto unaoteketeza mji huo utapanda juu
milele na milele!"
4 Na wale
wazee ishirini na wanne, na vile viumbe hai vinne, wakajitupa chini,
wakamwabudu Mungu aliyeketi juu ya kiti cha enzi wakisema, "Amina! Asifiwe
Mungu!"
5 Kisha
kukatokea sauti kwenye kiti cha enzi: "Msifuni Mungu enyi watumishi wake
wote, nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa."
6 Kisha
nikasikia kitu kama sauti ya umati mkubwa wa watu na sauti ya maji mengi na ya
ngurumo kubwa, ikisema, "Haleluya! Maana Bwana Mungu wetu Mwenye Uwezo ni
Mfalme!
7 Tufurahi
na kushangilia; tumtukuze, kwani wakati wa arusi ya Mwanakondoo umefika, na
bibi arusi yuko tayari.
8 Amepewa
uwezo wa kujivalia nguo ya kitani safi, iliyotakata na yenye kung`aa!"
(Nguo hiyo ya kitani safi ni matendo mema ya watu wa Mungu.)
9 Kisha
malaika akaniambia, "Andika haya: Heri wale walioalikwa kwenye karamu ya
arusi ya Mwanakondoo!" Tena akaniambia, "Hayo ni maneno ya kweli ya
Mungu."
10 Basi,
mimi nikaanguka kifudifudi mbele ya miguu yake nikataka kumwabudu. Lakini yeye
akaniambia, "Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako; sote
tunauzingatia ukweli ule alioufunua Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ukweli
alioufunua Yesu ndio unaowaangazia manabii."
11 Kisha
nikaona mbingu zimefunguliwa; na huko alikuwako farasi mmoja mweupe, na mpanda
farasi wake aliitwa "Mwaminifu" na "Kweli". Huyo huhukumu
na kupigana kwa ajili ya haki.
12 Macho
yake ni kama mwali wa moto, na alikuwa amevaa taji nyingi kichwani. Alikuwa
ameandikwa jina ambalo hakuna mtu alijuaye isipokuwa tu yeye mwenyewe.
13 Alikuwa
amevaa vazi lililokuwa limelowekwa katika damu. Na jina lake huyo ni "Neno
la Mungu."
14 Majeshi
ya mbinguni yalimfuata yakiwa yamepanda farasi weupe na walikuwa wamevaa mavazi
ya kitani, meupe na safi.
15 Upanga
mkali hutoka kinywani mwake, na kwa upanga huo atawashinda mataifa. Yeye ndiye
atakayetawala kwa fimbo ya chuma na kuikamua divai katika chombo cha kukamulia
zabibu za ghadhabu kuu ya Mungu Mwenye Uwezo.
16 Juu ya
vazi lake, na juu ya mguu wake, alikuwa ameandikwa jina: "Mfalme wa
wafalme na Bwana wa mabwana."
17 Kisha
nikamwona malaika mmoja amesimama katika jua. Akapaaza sauti na kuwaambia ndege
wote waliokuwa wanaruka juu angani, "Njoni! Kusanyikeni pamoja kwa karamu
kuu ya Mungu.
18 Njoni mkaitafune
miili ya wafalme, ya majemadari, ya watu wenye nguvu, ya farasi na wapanda
farasi wao; njoni mkaitafune miili ya watu wote: walio huru na watumwa, wadogo
na wakubwa."
19 Kisha
nikaona yule mnyama pamoja na mfalme wa dunia na askari wao wamekusanyika
pamoja kusudi wapigane na yule aliyekuwa ameketi juu ya farasi, pamoja na jeshi
lake.
20 Lakini
huyo mnyama akachukuliwa mateka, pamoja na nabii wa uongo aliyekuwa akifanya
miujiza mbele yake. (Kwa miujiza hiyo, alikuwa amewapotosha wale waliokuwa na
chapa ya huyo mnyama, na ambao walikuwa wameiabudu sanamu yake.) Huyo mnyama
pamoja na huyo nabii walitupwa wote wawili, wakiwa wazimawazima, ndani ya ziwa
linalowaka moto wa kiberiti.
21 Majeshi
yao yaliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule anayepanda farasi. Ndege
wote wakajishibisha kwa nyama zao.
|