Chapter 22
1 Kisha malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima maangavu kama
kioo yakitoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo.
2 Mto huo ulitiririka kupitia katikati ya barabara kuu ya
mji. Kandokando ya mto huo kulikuwa na mti wa uzima unaozaa matunda mara kumi
na mbili kwa mwaka, yaani kila mwezi; na majani yake ni dawa ya kuwaponya watu
wa mataifa.
3 Hapana kitu chochote kilicholaaniwa kitakachokuwa katika
mji huo. Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwa katika mji huo, na
watumishi wake watamwabudu.
4 Watauona uso wake, na jina lake litaandikwa juu ya paji
za nyuso zao.
5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa
au wa jua, maana Bwana Mungu atawaangazia, nao watatawala milele na milele.
6 Kisha malaika akaniambia, "Maneno haya ni ya kweli
na ya kuaminika. Bwana Mungu ambaye huwapa manabii Roho wake, alimtuma malaika
wake awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo lazima yatukie punde.
7
"Sikiliza! Naja upesi. Heri yake anayeyazingatia maneno ya unabii yaliyo
katika kitabu hiki."
8 Mimi
Yohane, niliyaona na kusikia mambo haya. Nilipokwisha sikia na kuona nikajitupa
chini mbele ya miguu ya huyo malaika aliyenionyesha mambo hayo, nikataka
kumwabudu.
9 Lakini
yeye akaniambia, "Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako
manabii na wote wanaoyatii maagizo yaliyomo katika kitabu hiki. Mwabudu
Mungu!"
10 Tena
akaniambia, "Usiyafiche kama siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu
hiki, maana wakati wa kutimizwa kwake umekaribia.
11 Kwa
sasa anayetenda mabaya na aendelee kutenda mabaya, na aliye mchafu aendelee
kuwa mchafu. Mwenye kutenda mema na azidi kutenda mema, na aliye mtakatifu na
azidi kuwa mtakatifu."
12
"Sikiliza!" Asema Yesu, "Naja upesi, pamoja na tuzo nitakalompa
kila mmoja kufuatana na matendo yake.
13 Mimi ni
Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, wa kwanza na wa mwisho."
14 Heri
yao wale wanaoosha mavazi yao, kwani watakuwa na haki ya kula tunda la mti wa
uzima, na haki ya kuingia mjini kwa kupitia milango yake.
15 Lakini
mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wote wanaopenda kusema uongo,
watakaa nje ya mji.
16
"Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu awathibitishieni mambo haya katika
makanisa. Mimi ni mzawa wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya
asubuhi!"
17 Roho na
Bibiarusi waseme, "Njoo!" Kila mtu asikiaye hili, na
aseme,"Njoo!" Kisha, yeyote aliye na kiu na aje; anayetaka maji ya
uzima na apokee bila malipo yoyote.
18 Mimi
Yohane nawapa onyo wote wanaosikia maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu
hiki: mtu yeyote akiongeza chochote katika mambo haya, Mungu atamwongezea mabaa
yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
19 Na mtu
yeyote akipunguza chochote katika maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki,
Mungu atamnyang`anya sehemu yake katika ule mti wa uzima, na sehemu yake katika
mji mtakatifu, ambavyo vimeelezwa katika kitabu hiki.
20 Naye
anayetoa ushahidi wake juu ya mambo haya asema: "Naam! Naja upesi."
Amina. Na iwe hivyo! Njoo Bwana Yesu!
21
Nawatakieni nyote neema ya Bwana Yesu. Amen.
|