Chapter 8
1 Yesu
aliposhuka kutoka mlimani, makundi mengi ya watu yalimfuata.
2 Basi,
akaja mtu mmoja mwenye ukoma, akamsujudia akisema, "Bwana, ukitaka, waweza
kunitakasa!"
3 Yesu akanyosha
mkono wake, akamgusa na kusema, "Nataka! Takasika." Mara huyo mtu
akapona ukoma wake.
4 Kisha
Yesu akamwambia, "Sikiliza, usimwambie mtu yeyote, ila nenda ukajionyeshe
kwa kuhani, na ukatoe sadaka iliyoamriwa na Mose kuwathibitishia kwamba
umepona."
5 Yesu
alipokuwa anaingia mjini Kafarnaumu, ofisa mmoja Mroma alimwendea, akamsihi
6 akisema,
"Mheshimiwa, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza na
anaumwa sana."
7 Yesu akamwambia,
"Nitakuja kumponya."
8 Huyo
ofisa akamwambia, "Mheshimiwa, sistahili uingie nyumbani mwangu. Lakini
sema tu neno, na mtumishi wangu atapona.
9 Maana,
hata mimi niliye mtu chini ya mamlaka ya wengine, ninao askari chini yangu.
Namwambia mmoja, `Nenda!` naye huenda; na mwingine, `Njoo!` naye huja; na
mtumishi wangu, `Fanya kitu hiki!` naye hufanya."
10 Yesu
aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia watu waliokuwa wanamfuata, "Kweli
nawaambieni, sijapata kumwona mtu yeyote katika Israeli aliye na imani kama
hii.
11 Basi,
nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao
wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika Ufalme wa
mbinguni.
12 Lakini
wale ambao wangalipaswa kuwa katika Ufalme huo watatupwa nje, gizani, ambako
watalia na kusaga meno."
13 Kisha
Yesu akamwambia huyo ofisa Mroma, "Nenda nyumbani; na iwe kama
ulivyoamini." Na mtumishi wake akapona saa ileile.
14 Yesu
alifika nyumbani kwa Petro, akamkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, ana
homa kali.
15 Basi,
Yesu akamgusa huyo mama mkono, na homa ikamwacha; akasimama, akamtumikia.
16
Ilipokuwa jioni, walimletea watu wengi waliokuwa wamepagawa na pepo; naye, kwa
kusema neno tu, akawafukuza hao pepo. Aliwaponya pia watu wote waliokuwa
wagonjwa.
17
Alifanya hivyo ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: "Yeye mwenyewe
ameondoa udhaifu wetu, ameyachukua magonjwa yetu."
18 Yesu
alipoona kundi la watu limemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake waende ng`ambo
ya ziwa.
19 Mwalimu
mmoja wa Sheria akamwendea, akamwambia, "Mwalimu, mimi nitakufuata kokote
uendako."
20 Yesu
akamjibu, "Mbweha wana mapango, na ndege wana viota; lakini Mwana wa Mtu
hana mahali pa kupumzikia."
21 Kisha
mtu mwingine miongoni mwa wanafunzi wake akamwambia, "Bwana, niruhusu
kwanza niende nikamzike baba yangu."
22 Lakini
Yesu akamwambia, "Nifuate! Waache wafu wazike wafu wao."
23 Yesu alipanda
mashua, na wanafunzi wake wakaenda pamoja naye.
24 Ghafla,
dhoruba kali ikatokea ziwani, hata mawimbi yakaanza kuifunika mashua. Yesu
alikuwa amelala usingizi.
25 Wanafunzi
wakamwendea, wakamwamsha wakisema, "Bwana, tuokoe, tunaangamia!"
26 Yesu
akawaambia, "Enyi watu wenye imani haba; mbona mnaogopa?" Basi,
akainuka, akazikemea pepo na mawimbi; kukawa shwari kabisa.
27 Watu
wakashangaa, wakasema, "Ni mtu wa namna gani huyu? Hata pepo na mawimbi
vinamtii!"
28 Yesu alifika
katika nchi ya Wagerasi,*fb* ng`ambo ya ziwa, na huko watu wawili waliopagawa
na pepo wakakutana naye wakitokea makaburini. Watu hawa walikuwa wenye kutisha
mno, hata hakuna mtu aliyethubutu kupita katika njia hiyo.
29 Nao wakaanza
kupiga kelele, "Una shauri gani nasi, wewe Mwana wa Mungu? Je, umekuja
kututesa kabla ya wakati wake?"
30 Karibu na
mahali hapo kulikuwa na nguruwe wengi wakichungwa.
31 Basi, hao
pepo wakamsihi, "Ikiwa utatutoa, basi uturuhusu tuwaingie nguruwe
wale."
32 Yesu
akawaambia, "Haya, nendeni." Hapo wakawatoka watu hao, wakawaingia
nguruwe. Kundi lote la nguruwe likaporomoka kwenye ule mteremko mkali,
likatumbukia ziwani; nguruwe wote wakafa maji.
33 Wachungaji wa
hao nguruwe walikimbia, wakaenda mjini. Huko walitoa habari zote na mambo yaliyowapata
wale watu waliokuwa wamepagawa.
34 Basi, watu
wote katika mji ule walitoka, wakamwendea Yesu; na walipomwona, wakamsihi
aondoke katika nchi yao.
|