Chapter 9
1 Yesu alipanda
mashua, akavuka ziwa na kufika katika mji wake.
2 Hapo watu
walimletea mtu mmoja aliyepooza mwili, amelazwa juu ya kitanda. Yesu alipoona
imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Jipe moyo mwanangu!
Umesamehewa dhambi zako."
3 Baadhi ya
walimu wa Sheria wakaanza kufikiri, "Mtu huyu anamkufuru Mungu!"
4 Yesu aliyajua
mawazo yao, akasema, "Kwa nini mnawaza mabaya mioyoni mwenu?
5 Ni lipi lililo
rahisi zaidi: kusema, `Umesamehewa dhambi zako`, au kusema, `Simama, utembee`?
6 Basi, nataka
mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kuwasamehe watu dhambi duniani."
Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Inuka, chukua kitanda chako, uende
nyumbani kwako."
7 Huyo mtu
aliyekuwa amepooza akainuka, akaenda nyumbani kwake.
8 Watu wote
katika ule umati walipoona hayo, walishangaa na kuogopa; wakamtukuza Mungu
aliyewapa binadamu uwezo wa namna hiyo.
9 Yesu aliondoka
hapo, na alipokuwa anakwenda zake, alimwona mtu mmoja aitwaye Mathayo, ameketi
katika ofisi ya ushuru. Basi, Yesu akamwambia, "Nifuate." Naye
Mathayo akainuka, akamfuata.
10 Yesu
alipokuwa nyumbani*fc* ameketi kula chakula, watoza ushuru wengi na wahalifu
walikuja wakaketi pamoja naye na wanafunzi wake.
11 Mafarisayo
walipoona hayo, wakawaambia wanafunzi wake, "Mbona mwalimu wenu anakula
pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?"
12 Yesu
aliwasikia, akasema, "Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni
wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, ila wenye dhambi.
13 Basi,
kajifunzeni maana ya maneno haya: `Nataka huruma, wala si dhabihu.` Sikuja
kuwaita watu wema, bali wenye dhambi."
14 Kisha
wanafunzi wa Yohane mbatizaji walimwendea Yesu, wakamwuliza, "Sisi na
Mafarisayo hufunga mara nyingi; mbona wanafunzi wako hawafungi?"
15 Yesu
akawajibu, "Je, walioalikwa arusini wanaweza kuomboleza wakati bwana arusi
yupo pamoja nao? La hasha! Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa
kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga.
16 "Hakuna
mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu. Maana kiraka hicho
kitararua hilo vazi kuukuu, na pale palipokuwa pameraruka pataongezeka.
17 Wala hakuna
mtu awekaye divai mpya katika viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, viriba hupasuka
na divai ikamwagika, navyo viriba vikaharibika. Ila divai mpya hutiwa katika
viriba vipya, na vyote viwili, viriba na divai, vikahifadhiwa salama."
18 Yesu
alipokuwa akisema hayo, ofisa mmoja Myahudi alifika, akamwinamia na kusema,
"Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini, tafadhali njoo umwekee mkono wako
naye ataishi."
19 Yesu
akaondoka pamoja na wanafunzi wake, akamfuata.
20 Mama mmoja,
mgonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, alimfuata Yesu nyuma,
akagusa pindo la vazi lake.
21 Alifanya
hivyo kwani alifikiri moyoni: "Nikigusa tu vazi lake, nitapona."
22 Basi, Yesu
akageuka akamwona, akamwambia, "Binti, jipe moyo! Imani yako
imekuponya." Mama huyo akapona saa ileile.
23 Kisha Yesu
akaingia nyumbani kwa yule ofisa. Na alipowaona wapiga filimbi na umati wa watu wanaofanya matanga,
24
akasema, "Ondokeni hapa! Msichana huyu hakufa, amelala tu." Nao
wakamcheka.
25 Basi,
umati wa watu ulipoondolewa, Yesu aliingia ndani, akamshika huyo msichana
mkono, naye akasimama.
26 Habari
hiyo ikavuma sana katika nchi ile yote.
27 Yesu
aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda, vipofu wawili walimfuata wakipiga
kelele, "Mwana wa Daudi, utuhurumie!"
28 Yesu
alipoingia nyumbani, vipofu hao wawili wakamwendea, naye akawauliza, "Je,
mnaamini kwamba naweza kuwafanyia jambo hilo?" Nao wakamjibu, "Naam,
Mheshimiwa."
29 Hapo
Yesu akayagusa macho yao, akasema, "Na iwe kwenu kama mnavyoamini."
30 Macho
yao yakafunguliwa. Naye Yesu akawaonya kwa ukali: "Msimwambie mtu yeyote
jambo hili."
31 Lakini
wao wakaondoka, wakaeneza habari za Yesu katika nchi ile yote.
32 Watu
walipokuwa wanakwenda zao, wengine walimletea Yesu mtu mmoja aliyekuwa bubu kwa
sababu alikuwa amepagawa na pepo.
33 Mara tu
huyo pepo alipotolewa, mtu huyo aliyekuwa bubu akaanza kuongea tena. Watu
wakashangaa na kusema, "Jambo kama hili halijapata kuonekana katika
Israeli!"
34 Lakini
Mafarisayo wakawa wanasema, "Anawatoa pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo
wabaya."
35 Yesu
alitembelea miji yote na vijiji, akafundisha katika masunagogi yao akihubiri
Habari Njema ya Ufalme wa Mungu, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila
namna.
36 Basi,
alipowaona watu, makundi kwa makundi, aliwaonea huruma kwa sababu walikuwa hoi
na wenye wasiwasi kama kondoo wasio na mchungaji.
37 Hapo
akawaambia wanafunzi wake, "Mavuno ni mengi, lakini wavunaji ni wachache.
38 Kwa
hivyo mwombeni mwenye shamba atume wavunaji shambani mwake."
|