Chapter 10
1 Yesu
aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa uwezo wa kutoa pepo wachafu na
kuponya magonjwa na maradhi yote.
2 Majina
ya hao mitume kumi na wawili ni haya: wa kwanza ni Simoni aitwae Petro, na
Andrea ndugu yake; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohane ndugu yake;
3 Filipo
na Bartholomayo, Thoma na Mathayo aliyekuwa mtoza ushuru; Yakobo mwana wa
Alfayo, na Thadayo;
4 Simoni Mkanaani, na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti
Yesu.
5 Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya:
"Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika mji wa
Wasamaria.
6 Ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo.
7 Mnapokwenda hubirini hivi: `Ufalme wa mbinguni umekaribia.`
8 Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma,
toeni pepo. Mmepewa bure, toeni bure.
9 Msichukue mifukoni mwenu dhahabu, wala fedha, wala sarafu
za shaba.
10 Msichukue mkoba wa kuombea njiani, wala koti la ziada,
wala viatu, wala fimbo. Maana mfanyakazi anastahili riziki yake.
11 "Mkiingia katika mji wowote au kijiji, tafuteni
humo mtu yeyote aliye tayari kuwakaribisheni, na kaeni naye mpaka mtakapoondoka
mahali hapo.
12 Mnapoingia nyumbani wasalimuni wenyeji wake.
13 Kama wenyeji wa nyumba hiyo wakiipokea salamu hiyo,
basi, amani yenu itakaa pamoja nao. Lakini ikiwa hawaipokei, basi amani yenu
itawarudia ninyi.
14 Kama mtu yeyote atakataa kuwakaribisheni au
kuwasikilizeni, basi mtokapo katika nyumba hiyo au mji huo, yakung`uteni
mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.
15 Kweli nawaambieni, Siku ya hukumu mji huo utapata adhabu
kubwa kuliko ile iliyoipata miji ya Sodoma na Gomora.
16 "Sasa, mimi nawatuma ninyi kama kondoo kati ya mbwa
mwitu. Muwe na busara kama nyoka, na wapole kama njiwa.
17 Jihadharini na watu, maana watawapeleka ninyi mahakamani
na kuwapiga viboko katika masunagogi yao.
18 Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu
yangu, mpate kutangaza Habari Njema kwao na kwa mataifa.
19 Basi, watakapowapeleka ninyi mahakamani, msiwe na
wasiwasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema.
20 Maana si ninyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu
asemaye ndani yenu.
21 "Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe, na baba
atamsaliti mwanawe, nao watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua.
22 Watu wote watawachukieni kwa sababu ya jina langu.
Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ataokolewa.
23 "Watu wakiwadhulumu katika mji mmoja, kimbilieni
mji mwingine. Kweli nawaambieni, hamtamaliza ziara yenu katika miji yote ya
Israeli kabla Mwana wa Mtu hajafika.
24 "Mwanafunzi si mkuu kuliko mwalimu wake, wala
mtumishi si mkuu kuliko bwana wake.
25 Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi
kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mkubwa wa jamaa Beelzebuli, je
hawatawaita watu wengine wa jamaa hiyo majina mabaya zaidi?
26
"Basi, msiwaogope watu hao. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila
kilichofichwa kitafichuliwa.
27
Ninalowaambieni ninyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo
mlilosikia likinong`onezwa, litangazeni hadharani.
28
Msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi
kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa
Jehanamu.
29 Shomoro
wawili huuzwa kwa senti tano. Lakini hata mmoja wao haanguki chini bila kibali
cha Baba yenu.
30 Lakini
kwa upande wenu, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.
31 Kwa
hiyo msiogope; ninyi mu wa thamani kuliko shomoro wengi. ic
32
"Kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri
mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.
33 Lakini
yeyote atakayenikana hadharani, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye
mbinguni.
34
"Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali
upanga.
35 Maana
nimekuja kuleta mafarakano kati ya mtu na baba yake, kati ya binti na mama
yake, kati ya mkwe na mkwe wake.
36 Na
maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake.
37
"Ampendaye baba au mama yake kuliko anipendavyo mimi, hanistahili.
Ampendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.
38 Mtu
asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili.
39
Anayeyashikilia maisha yake, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa
ajili yangu, atayapata.
40
"Anayewakaribisha ninyi, ananikaribisha mimi; na anayenikaribisha mimi,
anamkaribisha yule aliyenituma.
41
Anayemkaribisha nabii kwa sababu ni nabii, atapokea tuzo la nabii.
Anayemkaribisha mtu mwema kwa sababu ni mtu mwema, atapokea tuzo la mtu mwema.
42 Kweli
nawaambieni, yeyote atakayempa mmojawapo wa wadogo hawa kikombe cha maji baridi
kwa sababu ni mfuasi wangu, hatakosa kamwe kupata tuzo lake."
|