Chapter 11
1 Yesu
alipomaliza kuwapa wanafunzi kumi na wawili maagizo, alitoka hapo, akaenda
kufundisha na kuhubiri katika miji yao.
2 Yohane
mbatizaji akiwa gerezani alipata habari juu ya matendo ya Kristo. Basi, Yohane
akawatuma wanafunzi wake,
3
wamwulize: "Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?"
4 Yesu
akawajibu, "Nendeni mkamwambie Yohane mambo mnayoyasikia na kuyaona:
5 vipofu
wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa na viziwi wanasikia, wafu
wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema.
6 Heri mtu
yule asiyekuwa na mashaka nami."
7 Basi,
hao wajumbe wa Yohane walipokuwa wanakwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi
ya watu habari za Yohane: "Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je,
mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo?
8 Lakini
mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumtazama mtu aliyevaa mavazi maridadi? Watu
wanaovaa mavazi maridadi hukaa katika nyumba za wafalme.
9 Basi,
mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii.
10
"Huyu ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: `Tazama, hapa namtuma
mjumbe wangu, asema Bwana, akutangulie na kukutayarishia njia yako.`
11 Kweli
nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko
Yohane mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa
mbinguni, ni mkubwa kuliko yeye.
12 Tangu
wakati wa Yohane mbatizaji mpaka leo hii, Ufalme wa mbinguni unashambuliwa
vikali, na watu wakali wanajaribu kuunyakua kwa nguvu.
13
Mafundisho yote ya manabii na sheria yalibashiri juu ya nyakati hizi.
14 Kama mwaweza kukubali basi, Yohane ndiye
Eliya ambaye angekuja.
15 Mwenye
masikio na asikie!
16
"Basi, nitakifananisha kizazi hiki na kitu gani? Ni kama vijana waliokuwa
wamekaa uwanjani, wakawa wakiambiana kikundi kimoja kwa kingine:
17
`Tumewapigieni ngoma lakini hamkucheza; tumeimba nyimbo za huzuni lakini
hamkulia!`
18 Kwa
maana Yohane alikuja, akafunga na wala hakunywa divai, nao wakasema: `Amepagawa
na pepo.`
19 Mwana
wa Mtu akaja, anakula na kunywa, nao wakasema: `Mtazameni huyu, mlafi na mlevi,
rafiki yao watoza ushuru na wahalifu!` Hata hivyo, hekima ya Mungu
inathibitishwa kuwa njema kutokana na matendo yake."
20 Kisha
Yesu akaanza kuilaumu miji ambayo, ingawaje alifanya miujiza mingi humo, watu
wake hawakutaka kubadili nia zao mbaya:
21
"Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika
kwako ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya
gunia na kujipaka majivu zamani, ili kuonyesha kwamba wametubu.
22 Hata
hivyo nawaambieni, Siku ya hukumu, ninyi mtapata adhabu kubwa kuliko Tiro na
Sidoni.
23 Na wewe
Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka Kuzimu! Maana,
kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Sodoma, mji huo ungalikuwako
mpaka hivi leo.
24 Lakini
nawaambieni, Siku ya hukumu itakuwa nafuu zaidi kwa watu wa Sodoma, kuliko
kwako wewe."
25 Wakati
huo Yesu alisema, "Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana
umewaficha wenye hekima mambo haya, ukawafumbulia watoto wadogo.
26 Naam
Baba, ndivyo ilivyokupendeza.
27
"Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala
amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana atapenda kumjulisha.
28 Njoni
kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29
Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa
moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu.
30 Maana,
nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi."
|