Chapter 13
1 Siku hiyohiyo, Yesu alitoka katika ile nyumba, akaenda na
kuketi kando ya ziwa.
2 Makundi makubwa ya watu yalimzunguka hata Yesu akapanda
mashua, akaketi. Hao watu walisimama kwenye ukingo wa ziwa,
3 naye Yesu akawaambia mambo mengi kwa mifano.
"Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu.
4 Alipokuwa akipanda, nyingine zilianguka njiani, ndege
wakaja wakazila.
5 Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo
mwingi. Zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina.
6 Jua lilipochomoza, zilichomeka; na kwa kuwa mizizi yake
haikuwa na nguvu, zikanyauka.
7 Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na
kuzisonga.
8 Lakini nyingine zilianguka penye udongo mzuri, zikaota,
zikazaa: nyingine punje mia moja, nyingine sitini na nyingine thelathini.
9 Mwenye
masikio na asikie!"
10
Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwuliza, "Kwa nini unasema na watu kwa
mifano?"
11 Yesu
akawajibu, "Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za Ufalme wa mbinguni, lakini wao
hawakujaliwa.
12 Maana,
aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa; lakini yule asiye na kitu, hata kile
alicho nacho kitachukuliwa.
13 Ndiyo
maana ninasema nao kwa mifano, kwa sababu wanatazama lakini hawaoni,
wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawaelewi.
14 Kwao
yametimia yale aliyosema nabii Isaya: `Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa;
Kutazama mtatazama, lakini hamtaona.
15 Maana
akili za watu hawa zimepumbaa, wameyaziba masikio yao, wameyafumba macho yao.
La sivyo, wangeona kwa macho yao. wangesikia kwa masikio yao, wangeelewa kwa
akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya.`
16
"Lakini heri yenu ninyi, maana macho yenu yanaona na masikio yenu
yanasikia.
17 Kweli
nawaambieni, manabii na watu wengi wema walitamani kuyaona yale mnayoyaona,
wasiyaone, na kuyasikia yale mnayoyasikia, wasiyasikie.
18
"Basi, ninyi sikilizeni maana ya mfano huo wa mpanzi.
19 Yeyote
asikiaye ujumbe wa ufalme bila kuuelewa, ni kama zile mbegu zilizoanguka
njiani; yule Mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake.
20 Ile
mbegu iliyopandwa penye mawe ni mfano wa mtu asikiaye ujumbe huo na mara
akaupokea kwa furaha.
21 Lakini
haumwingii na kuwa na mizizi ndani yake; huendelea kuuzingatia ujumbe huo kwa
kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya ujumbe huo,
anakata tamaa mara.
22 Ile
mbegu iliyoanguka kati ya miti ya miiba, ni mfano wa mtu asikiaye huo ujumbe,
lakini wasiwasi wa ulimwengu huu na anasa za mali huusonga ujumbe huo, naye
hazai matunda.
23 Ile
mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri ni mfano wa mtu ausikiaye ujumbe huo na
kuuelewa, naye huzaa matunda; mmoja mia, mwingine sitini na mwingine
thelathini."
24 Yesu
akawaambia watu mfano mwingine: "Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu
aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake.
25 Lakini
watu wakiwa wamelala, adui yake akaja akapanda magugu kati ya ngano, akaenda
zake.
26 Basi,
mimea ilipoota na kuanza kuchanua, magugu pia yakaanza kuonekana.
27
Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwambia, `Mheshimiwa, bila
shaka ulipanda mbegu nzuri katika shamba lako. Sasa magugu yametoka wapi?`
28 Yeye
akawajibu, `Adui ndiye aliyefanya hivyo.` Basi, watumishi wake wakamwuliza,
`Je, unataka twende tukayang`oe`
29 Naye
akawajibu, `La, msije labda mnapokusanya magugu, mkang`oa na ngano pia.
30 Acheni
vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji: kusanyeni
kwanza magugu mkayafunge mafungumafungu ya kuchomwa. Lakini ngano ikusanyeni
mkaiweke ghalani mwangu."`
31 Yesu
akawaambia watu mfano mwingine: "Ufalme wa mbinguni unafanana na mbegu ya
haradali aliyotwaa mtu mmoja, akaipanda katika shamba lake.
32 Yenyewe
ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini ikishaota huwa kubwa kuliko mimea yote.
Hukua ikawa mti, na ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake."
33 Yesu
akawaambia mfano mwingine: "Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu
aliyotwaa mama mmoja, akaichanganya na unga pishi tatu, hata unga wote
ukaumuka."
34 Yesu
aliwaambia watu hayo yote kwa mifano. Hakuwaambia chochote bila kutumia
mifano,
35 ili jambo lililonenwa na nabii litimie: "Nitasema
kwa mifano; nitawaambia mambo yaliyofichika tangu kuumbwa ulimwengu."
36 Kisha Yesu aliwaaga wale watu, akaingia nyumbani.
Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, "Tufafanulie ule mfano wa magugu
shambani."
37 Yesu akawaambia, "Mpanzi wa zile mbegu nzuri ni
Mwana wa Mtu.
38 Lile shamba ni ulimwengu. Zile mbegu nzuri ni watu wale
ambao Ufalme ni wao. Lakini yale magugu ni wale watu wa yule Mwovu.
39 Adui aliyepanda yale magugu ni Ibilisi. Mavuno ni mwisho
wa nyakati na wavunaji ni malaika.
40 Kama vile magugu yanavyokusanywa kuchomwa moto, ndivyo
itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati;
41 Mwana wa Mtu atawatuma malaika wake wawakusanye kutoka
katika Ufalme wake wale wote wenye kusababisha dhambi, na wote wenye kutenda
maovu,
42 na
kuwatupa katika tanuru ya moto, na huko watalia na kusaga meno.
43 Kisha,
wale wema watang`ara kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Sikieni basi, kama mna
masikio!
44
"Ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja
aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa
nayo, akalinunua shamba lile.
45
"Tena, Ufalme wa mbinguni umefanana na mfanyabiashara mmoja mwenye
kutafuta lulu nzuri.
46
Alipopata lulu moja ya thamani kubwa, alienda akauza yote aliyokuwa nayo,
akainunua lulu ile.
47
"Tena, Ufalme wa mbinguni unafanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa
samaki wa kila aina.
48
Ulipojaa, watu waliuvuta pwani, wakaketi, wakachagua samaki wazuri wakawaweka
ndani ya vikapu vyao, na wabaya wakawatupa.
49 Ndivyo
itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati: malaika watatokea, watawatenganisha watu
wabaya na watu wema,
50 na
kuwatupa hao wabaya katika tanuru ya moto. Huko watalia na kusaga meno."
51 Yesu
akawauliza, "Je, mmeelewa mambo haya yote?" Wakamjibu,
"Naam."
52 Naye
akawaambia, "Hivyo basi, kila mwalimu wa Sheria aliye mwanafunzi wa Ufalme
wa mbinguni anafanana na mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na
vya kale."
53 Yesu
alipomaliza kusema mifano hiyo alitoka mahali hapo,
54 akaenda
kijijini kwake. Huko akawa anawafundisha watu katika sunagogi hata wakashangaa,
wakasema, "Huyu amepata wapi hekima hii na maajabu?
55 Je,
huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake
si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda?
56 Na dada
zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi amepata wapi haya yote?"
57 Basi,
wakawa na mashaka naye. Lakini Yesu akawaambia, "Nabii hakosi kuheshimiwa,
isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake!"
58 Kwa
hiyo, hakutenda miujiza mingi pale kwa sababu ya kutoamini kwao.
|