Chapter 14
1 Wakati
huo, mtawala Herode alisikia sifa za Yesu.
2 Basi,
akawaambia watumishi wake, "Mtu huyu ni Yohane mbatizaji, amefufuka kutoka
wafu; ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake."
3 Herode
ndiye aliyekuwa amemtia Yohane nguvuni, akamfunga minyororo na kumtia gerezani
kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake. Sababu hasa ni
4 kwamba
alikuwa amemwambia Herode, "Si halali kwako kuishi na huyo mwanamke!"
5 Herode
alitaka kumwua Yohane, lakini aliogopa watu kwa sababu kwao Yohane alikuwa
nabii.
6 Katika
sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya
wageni. Herode alifurahiwa,
7 hata
akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba.
8 Naye,
huku akichochewa na mama yake, akaomba, "Nipe papahapa katika sinia kichwa
cha Yohane mbatizaji."
9 Mfalme
alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni
karamuni, akaamuru apewe.
10 Basi,
Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane.
11 Kichwa
chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama
yake.
12
Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda
kumpasha habari Yesu.
13 Yesu
alipopata habari hiyo, aliondoka mahali pale kwa mashua, akaenda mahali pa
faragha peke yake. Lakini watu walipata habari, wakamfuata kwa miguu toka
mijini.
14 Basi,
aliposhuka pwani, aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, akawaponya
wagonjwa wao.
15
Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea wakamwambia, "Mahali hapa ni
nyikani, na saa zimepita. Basi, uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie
chakula."
16 Yesu
akawaambia, "Si lazima waende, wapeni ninyi chakula."
17 Lakini
wao wakamwambia, "Tunayo mikate mitano tu na samaki wawili."
18 Yesu
akawaambia, "Nileteeni hapa."
19
Akawaamuru watu waketi katika nyasi. Kisha akaitwaa ile mikate mitano na wale
samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu. Halafu akaimega hiyo
mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu.
20 Watu
wote wakala, wakashiba. Kisha wanafunzi wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu
kumi na viwili.
21 Jumla
ya waliokula ilikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na
watoto.
22 Mara,
Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie ng`ambo ya ziwa
wakati yeye anawaaga watu.
23 Baada
ya kuwaaga, alipanda mlimani peke yake kusali. Ilipokuwa jioni, yeye alikuwa
huko peke yake,
24 na
wakati huo ile mashua ilikwishafika karibu katikati ya ziwa, lakini ilikuwa
inakwenda mrama kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga.
25 Usiku,
karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji.
26
Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji waliingiwa na hofu, wakasema,
"Ni mzimu!" Wakapiga kelele kwa hofu.
27 Mara,
Yesu akasema nao, "Tulieni, ni mimi. Msiogope!"
28 Petro
akamwambia, "Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije
kwako."
29 Yesu
akasema, "Haya, njoo." Basi, Petro akashuka kutoka ile mashua,
akatembea juu ya maji, akamwendea Yesu.
30 Lakini
alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, "Bwana,
niokoe!"
31 Hapo,
Yesu akaunyosha mkono wake, akamshika na kumwambia, "Ewe mwenye imani
haba! Kwa nini uliona shaka?"
32 Basi,
wakapanda mashuani, na upepo ukatulia.
33 Wote
waliokuwa ndani ya mashua walimsujudia, wakasema, "Hakika wewe ni Mwana wa
Mungu."
34
Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti.
35 Watu wa
huko walipomtambua, wakaeneza habari pote katika sehemu hizo. Basi, wakamletea
Yesu wagonjwa wote,
36
wakamwomba awaruhusu waguse tu pindo la vazi lake; wote waliomgusa walipona.
|