Chapter 15
1 Kisha
Mafarisayo na walimu wa Sheria wakafika kutoka Yerusalemu, wakamwendea Yesu,
wakamwuliza,
2
"Kwa nini wanafunzi wako hawajali mapokeo tuliyopokea kutoka kwa wazee
wetu? Hawanawi mikono yao kama ipasavyo kabla ya kula!"
3 Yesu
akawajibu, "Kwa nini nanyi mnapendelea mapokeo yenu wenyewe na hamuijali
Sheria ya Mungu?
4 Mungu
amesema: `Waheshimu baba yako na mama yako,` na `Anayemkashifu baba yake au
mama yake, lazima auawe`.
5 Lakini
ninyi mwafundisha ati mtu akiwa na kitu ambacho angeweza kuwasaidia nacho baba
au mama yake, lakini akasema: `Kitu hiki nimemtolea Mungu,`
6 basi,
hapaswi tena kumheshimu baba yake! Ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa
kufuata mafundisho yenu wenyewe.
7 Enyi
wanafiki! Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu:
8 `Watu
hawa, asema Mungu, huniheshimu kwa maneno tu, lakini mioyoni mwao wako mbali
nami.
9
Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu
tu."`
10 Yesu
aliuita ule umati wa watu, akawaambia, "Sikilizeni na muelewe!
11 Kitu
kinachomtia mtu najisi si kile kiingiacho kinywani, bali kile kitokacho
kinywani. Hicho ndicho kimtiacho mtu najisi."
12 Kisha
wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, "Je, unajua kwamba Mafarisayo
walichukizwa waliposikia maneno yako?"
13 Lakini
yeye akawajibu, "Kila mmea ambao Baba yangu aliye mbinguni hakuupanda,
utang`olewa.
14
Waacheni wenyewe! Wao ni vipofu, viongozi wa vipofu; na kipofu akimwongoza
kipofu, wote wawili hutumbukia shimoni."
15 Petro
akadakia, "Tufafanulie huo mfano."
16 Yesu
akasema, "Hata nyinyi hamwelewi?
17 Je,
hamwelewi kwamba kila kinachoingia kinywani huenda tumboni na baadaye hutupwa
nje chooni?
18 Lakini
yale yatokayo kinywani hutoka moyoni, na hayo ndiyo yanayomtia mtu najisi.
19 Maana
moyoni hutoka mawazo maovu yanayosababisha uuaji, uzinzi, uasherati, wizi,
ushahidi wa uongo na kashfa.
20 Hayo
ndiyo yanayomtia mtu najisi. Lakini kula chakula bila kunawa mikono hakumtii
mtu najisi."
21 Yesu
aliondoka mahali hapo akaenda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni.
22 Basi,
mama mmoja Mkaanani wa nchi hiyo alimjia, akapaaza sauti: "Mheshimiwa,
Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo."
23 Lakini
Yesu hakumjibu neno. Basi, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, "Mwambie
aende zake kwa maana anatufuatafuata akipiga kelele."
24 Yesu
akajibu, "Sikutumwa ila kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo."
25 Hapo
huyo mama akaja, akapiga magoti mbele yake, akasema, "Mheshimiwa,
nisaidie."
26 Yesu
akamjibu, "Si sawa kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa."
27 Huyo
mama akajibu, "Ni kweli, Mheshimiwa; lakini hata mbwa hula makombo
yanayoanguka kutoka meza ya bwana wao."
28 Hapo
Yesu akamjibu, "Mama, imani yako ni kubwa; basi, ufanyiwe kama unavyotaka." Yule binti yake
akapona tangu saa hiyo wakati huohuo.
29 Yesu
alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi.
30 Watu
wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi
waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya.
31 Umati
ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa
wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; wakamsifu Mungu wa
Israeli.
32 Basi,
Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, "Nawaonea watu hawa huruma kwa
sababu kwa siku tatu wamekuwa nami, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha
waende bila kula wasije wakazimia njiani."
33
Wanafunzi wakamwambia, "Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha
kuwatosha watu wengi hivi?"
34 Yesu
akawauliza, "Mnayo mikate mingapi?" Wakamjibu, "Saba na visamaki vichache."
35 Basi, Yesu
akawaamuru watu wakae chini.
36
Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akamshukuru Mungu, akavimega,
akawapa wanafunzi, nao wakawagawia watu.
37 Wote
wakala, wakashiba. Kisha wakakusanya makombo, wakajaza vikapu saba.
38 Hao
waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto.
39 Basi,
Yesu akawaaga watu, akapanda mashua, akaenda katika eneo la Magadani.
|