Chapter 16
1
Mafarisayo na Masadukayo walimwendea Yesu, na kwa kumjaribu, wakamwomba afanye
ishara itokayo mbinguni.
2 Lakini
Yesu akawajibu, "Wakati wa jioni ukifika ninyi husema: `Hali ya hewa
itakuwa nzuri kwa maana anga ni jekundu!`
3 Na
alfajiri mwasema: `Leo hali ya hewa itakuwa ya dhoruba, maana anga ni jekundu
na tena mawingu yametanda!` Basi, ninyi mnajua sana kusoma majira kwa kuangalia anga,
lakini kutambua dalili za nyakati hizi hamjui.
4 Kizazi
kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara, lakini hamtapewa ishara yoyote
isipokuwa tu ile ya Yona." Basi, akawaacha, akaenda zake.
5
Wanafunzi wake walipokwisha vukia upande wa pili wa ziwa, walijikuta wamesahau
kuchukua mikate.
6 Yesu
akawaambia, "Muwe macho na mjihadhari na chachu ya Mafarisayo na
Masadukayo!"
7 Lakini
wao wakawa wanajadiliana: "Anasema hivyo kwa kuwa hatukuchukua
mikate."
8 Yesu
alijua mawazo yao, akawaambia, "Enyi watu wenye imani haba! Mbona
mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate?
9 Je,
hamjaelewa bado? Je, hamkumbuki nilipoimega ile mikate mitano kwa ajili ya wale
watu elfu tano? Je, mlijaza vikapu vingapi vya makombo?
10 Au, ile
mikate saba waliyogawiwa wale watu elfu nne, je, mlikusanya vikapu vingapi vya
mabaki?
11
Inawezekanaje hamwelewi ya kwamba sikuwa nikisema juu ya mikate? Jihadharini na
chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!"
12 Hapo
wanafunzi wakafahamu kwamba aliwaambia wajihadhari siyo na chachu ya mikate,
bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
13 Yesu
alipofika pande za Kaisarea Filipi, aliwauliza wanafunzi wake, "Watu
wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?"
14
Wakamjibu, "Wengine wanasema kuwa ni Yohane mbatizaji, wengine Eliya,
wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii."
15 Yesu
akawauliza, "Na ninyi je, mwasema mimi ni nani?"
16 Simoni
Petro akajibu, "Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai."
17 Yesu
akasema, "Heri wewe Simoni mwana wa Yona, kwa maana si binadamu
aliyekufunulia ukweli huu, ila Baba yangu aliye mbinguni.
18 Nami
nakwambia: wewe ni Petro, na juu ya mwamba*ff* huu nitalijenga kanisa langu;
wala kifo chenyewe hakitaweza kulishinda.
19
Nitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni; kila utakachofunga duniani, kitafungwa
pia mbinguni; kila utakachofungua duniani, kitafunguliwa pia mbinguni."
20 Kisha
akawaonya wanafunzi wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Kristo.
21 Tangu
wakati huo Yesu alianza kuwajulisha waziwazi wanafunzi wake: "Ni lazima
mimi niende Yerusalemu, na huko nikapate mateso mengi yatakayosababishwa na
wazee, makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Nitauawa, na siku ya tatu
nitafufuliwa."
22 Hapo
Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea: "Isiwe hivyo Bwana! Jambo hili
halitakupata!"
23 Lakini
Yesu akageuka, akamwambia Petro, "Ondoka mbele yangu Shetani! Wewe ni
kikwazo kwangu. Mawazo yako si ya mungu bali ni ya kibinadamu!"
24 Kisha
Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kama mtu yeyote anataka kuwa mfuasi
wangu, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.
25 Maana,
mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza;
26 lakini
mtu anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata. Je, mtu atafaidi nini
akiupata utajiri wote wa ulimwengu na hali amepoteza maisha yake? Au, mtu
atatoa kitu gani kiwe badala ya maisha yake?
27 Maana,
Mwana wa Mtu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika wake, na
hapo ndipo atakapomlipa kila mtu kadiri ya matendo yake.
28 Kweli
nawaambieni, wako wengine papahapa ambao hawatakufa kabla ya kumwona Mwana wa
Mtu akija katika Ufalme wake."
|