Chapter 19
1 Yesu
alipomaliza kusema maneno hayo, alitoka Galilaya, akaenda katika mkoa wa Yudea,
ng`ambo ya mto Yordani.
2 Watu
wengi walimfuata huko, naye akawaponya.
3
Mafarisayo kadhaa walimjia, wakamwuliza kwa kumtega, "Je, ni halali mume
kumpa talaka mkewe kwa kisa chochote?"
4 Yesu
akawajibu, "Je, hamkusoma katika Maandiko Matakatifu kwamba Mungu aliyemuumba
mtu tangu mwanzo alimfanya mwanamume na mwanamke,
5 na
akasema: `Kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, ataungana
na mke wake, nao wawili watakuwa mwili mmoja?`
6 Kwa hiyo wao si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi,
alichounganisha Mungu, binadamu asikitenganishe."
7 Lakini wao wakamwuliza, "Kwa nini basi, Mose
alituagiza mwanamke apewe hati ya talaka na kuachwa?"
8 Yesu akawajibu, "Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu
kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu.
9 Lakini haikuwa hivyo tangu mwanzo. Basi nawaambieni,
yeyote atakayemwacha mke wake isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, akaoa mke
mwingine, anazini."
10 Wanafunzi wake wakamwambia, "Ikiwa mambo ya mume na
mkewe ni hivyo, ni afadhali kutooa kabisa."
11 Yesu akawaambia, "Si wote wanaoweza kulipokea
fundisho hili, isipokuwa tu wale waliojaliwa na Mungu.
12 Maana kuna sababu kadhaa za kutoweza kuoa: wengine ni
kwa sababu wamezaliwa hivyo, wengine kwa sababu wamefanywa hivyo na watu, na
wengine wameamua kutooa kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea
fundisho hili na alipokee."
13 Kisha watu wakamletea Yesu watoto wadogo ili awawekee
mikono na kuwaombea. Lakini wanafunzi wakawakemea.
14 Yesu akasema, "Waacheni hao watoto waje kwangu,
wala msiwazuie; maana Ufalme wa mbinguni ni wa watu walio kama watoto
hawa."
15 Basi, akawawekea mikono, kisha akaondoka mahali hapo.
16 Mtu mmoja alimjia Yesu, akamwuliza, "Mwalimu,
nifanye kitu gani chema ili niupate uzima wa milele?"
17 Yesu akamwambia, "Mbona unaniuliza kuhusu jambo
jema? Kuna mmoja tu aliye mwema. Ukitaka kuingia katika uzima, shika
amri."
18 Yule mtu akamwuliza, "Amri zipi?" Yesu
akasema, "Usiue, usizini, usiibe, usitoe ushahidi wa uongo,
19 waheshimu baba yako na mama yako; na, mpende jirani yako
kama unavyojipenda mwenyewe."
20 Huyo kijana akamwambia, "Hayo yote nimeyazingatia
tangu utoto wangu; sasa nifanye nini zaidi?"
21 Yesu akamwambia, "Kama unapenda kuwa mkamilifu,
nenda ukauze mali yako uwape maskini hiyo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni,
kisha njoo unifuate."
22 Huyo kijana aliposikia hayo, alienda zake akiwa mwenye
huzuni, maana alikuwa na mali nyingi.
23 Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kweli
nawaambieni, itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni.
24 Tena nawaambieni, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita
katika tundu la sindano, kuliko kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa
mbinguni."
25 Wale wanafunzi waliposikia hivyo walishangaa, wakamwuliza,
"Ni nani basi, awezaye kuokoka?"
26 Yesu akawatazama, akasema, "Kwa binadamu jambo hili
haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana."
27 Kisha
Petro akasema, "Na sisi je? Tumeacha yote tukakufuata; tutapata nini
basi?"
28 Yesu
akawaambia, "Nawaambieni kweli, Mwana wa Mtu atakapoketi katika kiti cha
enzi cha utukufu wake katika ulimwengu mpya, ninyi mlionifuata mtaketi katika
viti kumi na viwili mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.
29 Na kila
aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au baba, au mama, au watoto, au mashamba,
kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi, na kupata uzima wa milele.
30 Lakini
walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.
|