Chapter 20
1
"Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba la mizabibu, ambaye
alitoka asubuhi na mapema kuwaajiri wafanyakazi katika shamba lake.
2
Akapatana nao kuwalipa dinari moja kwa siku, kisha akawapeleka katika shamba
lake la mizabibu.
3 Akatoka
mnamo saa tatu asubuhi, akaona watu wengine wamesimama sokoni, hawana kazi.
4
Akawaambia, `Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu, nami
nitawapeni haki yenu.`
5 Basi, wakaenda. Huyo mwenye shamba akatoka tena mnamo saa
sita na saa tisa, akafanya vivyo hivyo.
6 Hata mnamo saa kumi na moja jioni, akatoka tena; akakuta
watu wengine wamesimama pale sokoni. Basi, akawauliza, `Mbona mmesimama hapa
mchana kutwa bila kazi?`
7 Wakamjibu: `Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri.` Yeye
akawaambia, `Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu.`
8 "Kulipokuchwa, huyo mwenye shamba alimwambia mtunza
hazina wake, `Waite wafanyakazi ukawalipe mshahara wao, ukianzia na wale
walioajiriwa mwisho, na kumalizia na wale wa kwanza.`
9 Basi, wakaja wale walioajiriwa mnamo saa kumi na moja,
wakapokea kila mmoja dinari moja.
10 Wale wa kwanza walipofika, walikuwa wanadhani watapewa
zaidi; lakini hata wao wakapewa kila mmoja dinari moja.
11 Wakazipokea fedha zao, wakaanza kumnung`unikia yule bwana.
12 Wakasema, `Watu hawa walioajiriwa mwisho walifanya kazi
kwa muda wa saa moja tu, mbona umetutendea sawa na wao hali sisi tumevumilia
kazi ngumu kutwa na jua kali?`
13 "Hapo yule bwana akamjibu mmoja wao, `Rafiki, sikukupunja
kitu! Je, hukupatana nami mshahara wa denari moja?
14 Chukua haki yako, uende zako. Napenda kumpa huyu wa
mwisho sawa na wewe.
15 Je, sina haki ya kufanya na mali yangu nipendavyo? Je,
unaona kijicho kwa kuwa mimi ni mwema?"`
16 Yesu akamaliza kwa kusema, "Hivyo, walio wa mwisho
watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho."
17 Yesu alipokuwa anakwenda Yerusalemu, aliwachukua wale
wanafunzi kumi na wawili faraghani, na njiani akawaambia,
18 "Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana
wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na walimu wa Sheria, nao watamhukumu
auawe.
19 Watamkabidhi kwa watu wa mataifa mengine ili adhihakiwe,
apigwe viboko na kusulubiwa; lakini siku ya tatu atafufuliwa."
20 Hapo mama yao wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na
wanawe, akapiga magoti mbele yake na kumwomba kitu.
21 Yesu akamwuliza, "Unataka nini?" Huyo mama
akamwambia, "Ahidi kwamba katika Ufalme wako, hawa wanangu wawili watakaa
mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto."
22 Yesu akajibu, "Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza
kunywa kikombe nitakachokunywa mimi?" Wakamjibu, "Tunaweza."
23 Yesu akawaambia, "Kweli mtakunywa kikombe changu,
lakini kuketi kulia au kushoto kwangu si kazi yangu kupanga; jambo hilo
watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu."
24 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia
hao ndugu wawili.
25 Hivyo Yesu akawaita, akawaambia, "Mnajua kwamba
watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu na wakuu hao huwamiliki watu
wao.
26 Lakini kwenu isiwe hivyo, ila yeyote anayetaka kuwa mkuu
kati yenu sharti awe mtumishi wa wote;
27 na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe
mtumishi wenu.
28 Jinsi hiyohiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali
kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi."
29 Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu
ulimfuata.
30 Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia,
na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaaza sauti:
"Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!"
31 Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze.
Lakini wao wakazidi kupaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi,
utuhurumie!"
32 Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, "Mnataka
niwafanyie nini?"
33 Wakamjibu, "Mheshimiwa, tunaomba macho yetu
yafumbuliwe."
34 Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na
papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata.
|