Chapter 24
1 Yesu
alitoka Hekaluni, na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake walimwendea,
wakamwonyesha majengo ya Hekalu.
2 Yesu
akawaambia, "Sawa, mnaweza kuyatazama haya yote! Kweli nawaambieni, hakuna
hata jiwe moja litakalosalia hapa juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa."
3 Yesu
alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni, wanafunzi walimwendea faraghani,
wakamwuliza, "Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani
itakayoonyesha kuja kwako na mwisho wa nyakati?"
4 Yesu
akawajibu, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu.
5 Maana
wengi watatokea na kulitumia jina langu wakisema: `Mimi ndiye Kristo,` nao
watawapotosha watu wengi.
6 Mtasikia
juu ya vita na fununu za vita; lakini msifadhaike, maana hayo hayana budi
kutokea, lakini mwisho wenyewe ungali bado.
7 Taifa
moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine.
Hapa na pale patakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi.
8 Yote
hayo ni kama mwanzo wa maumivu ya kujifungua mtoto.
9
"Kisha watawatoeni ili mteswe na kuuawa. Mataifa yote yatawachukieni kwa
ajili ya jina langu.
10 Tena,
wengi wataiacha imani yao, watasalitiana na kuchukiana.
11
Watatokea manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu wengi.
12 Kwa
sababu ya ongezeko la uhalifu, upendo wa watu wengi utafifia.
13 Lakini
atakayevumilia mpaka mwisho, ataokoka.
14 Ila,
kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya Ufalme wa Mungu itahubiriwa
ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote.
15
"Basi, mtakapoona `Chukizo Haribifu` lililonenwa na nabii Danieli
limesimama mahali patakatifu, (msomaji na atambue maana yake),
16 hapo, walioko Yudea na wakimbilie milimani.
17 Aliye juu ya paa la nyumba yake asishuke kuchukua kitu
nyumbani mwake.
18 Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.
19 Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku
hizo!
20 Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe siku za baridi au siku
ya Sabato!
21 Maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata
kuwako tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka leo, wala haitapata kutokea tena.
22 Kama siku hizo hazingalipunguzwa, hakuna binadamu yeyote
ambaye angeokoka; lakini siku hizo zitapunguzwa kwa ajili ya wale walioteuliwa.
23 "Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: `Kristo yuko
hapa` au `Yuko pale,` msimsadiki.
24 Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa
uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata
wateule wa Mungu.
25 Sikilizeni, nimekwisha kuwaonya kabla ya wakati.
26 Basi, wakiwaambieni, `Tazameni, yuko jangwani,` msiende
huko; au, `Tazameni, amejificha ndani,` msisadiki;
27 maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi
magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.
28 Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
29 "Mara baada ya dhiki ya siku hizo, jua litatiwa
giza, mwezi hautaangaza, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu
zitatikiswa.
30 Kisha, ishara ya Mwana wa Mtu itaonekana angani, na hapo
makabila yote duniani yatalalamika; watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu
ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi.
31 Naye atawatuma malaika wake wenye tarumbeta la kuvuma
sana, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, toka
mwisho huu wa mbingu hadi mwisho huu.
32 "Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake
yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi
umekaribia.
33 Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo haya yote
yakitendeka, jueni kwamba yuko karibu sana.*fk*
34 Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo
hayo yote kutukia.
35 Naam, mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu
hayatapita kamwe.
36 "Lakini, juu ya siku au saa hiyo, hakuna mtu ajuaye
itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake ndiye
ajuaye.
37 Kwa maana kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo
itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.
38 Maana nyakati hizo, kabla ya gharika kuu, watu walikuwa
wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka Noa alipoingia ndani ya ile safina.
39 Hawakujua kuna nini mpaka ile gharika ilipotokea,
ikawakumba wote. Ndivyo itakavyokuwa wakati Mwana wa Mtu atakapokuja.
40 Wakati huo watu wawili watakuwa shambani; mmoja
atachukuliwa na mwingine ataachwa.
41 Kina mama wawili watakuwa wanasaga nafaka, mmoja
atachukuliwa na mwingine ataachwa.
42 Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu.
43 Lakini kumbukeni jambo hili: kama mwenye nyumba angejua
siku mwizi atakapofika, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe.
44 Kwa hiyo, nanyi pia muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu
atakuja saa msiyoitazamia."
45 Yesu akaendelea kusema, "Ni nani basi mtumishi
mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watu wake, awape
chakula kwa wakati wake?
46 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakapokuja
atamkuta akifanya hivyo.
47 Kweli nawaambieni, atamweka mtumishi huyo aisimamie mali
yake yote.
48 Lakini kama mtumishi mbaya akijisemea moyoni: `Bwana
wangu anakawia kurudi,`
49 kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, akaanza kula
na kunywa pamoja na walevi,
50 bwana wake atakuja siku asiyoitazamia na saa asiyoijua.
51
Atamkatilia mbali na kumweka kundi moja na wanafiki. Huko kutakuwa na kilio na
kusaga meno.
|