Chapter 25
1
"Wakati huo, Ufalme wa mbinguni utafanana na wasichana kumi waliochukua
taa zao, wakaenda kumlaki bwana arusi.
2 Watano miongoni
mwao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara.
3 Wale
wapumbavu walichukua taa zao, lakini hawakuchukua akiba ya mafuta.
4 Lakini
wale wenye busara walichukua mafuta katika chupa pamoja na taa zao.
5 Kwa kuwa
bwana arusi alikawia kuja, wale wanawali wote wote walisinzia, wakalala.
6 Usiku wa
manane kukawa na kelele: `Haya, haya! Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.`
7 Hapo
wale wanawali wote wakaamka, wakazitayarisha taa zao.
8 Wale
wapumbavu wakawaambia wale wenye busara: `Tupeni mafuta yenu kidogo maana taa
zetu zinazimika.`
9 Lakini
wale wenye busara wakawaambia, `Hayatatutosha sisi na ninyi! Afadhali mwende
dukani mkajinunulie wenyewe!`
10 Basi,
wale wanawali wapumbavu walipokwenda kununua mafuta, bwana arusi akafika, na
wale wanawali waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye katika jumba la arusi,
kisha mlango ukafungwa.
11 Baadaye
wale wanawali wengine wakaja, wakaita: `Bwana, bwana, tufungulie!`
12 Lakini
yeye akawajibu, `Nawaambieni kweli, siwajui ninyi."`
13 Kisha
Yesu akasema, "Kesheni basi, kwa maana hamjui siku wala saa.
14
"Itakuwa kama mtu mmoja aliyetaka kusafiri ng`ambo: aliwaita watumishi
wake, akawakabidhi mali yake.
15 Alimpa
kila mmoja kadiri ya uwezo wake: mmoja sarafu tano za fedha ziitwazo talanta,
mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kisha akasafiri.
16 Mara
yule aliyekabidhiwa talanta tano akafanya kazi nazo akapata faida talanta tano.
17 Hali
kadhalika na yule aliyekabidhiwa talanta mbili akapata faida talanta mbili.
18 Lakini
yule aliyekabidhiwa talanta moja akaenda akachimba shimo ardhini, akaificha
fedha ya bwana wake.
19
"Baada ya muda mrefu, yule bwana alirudi, akaanza kukagua hesabu ya
matumizi na mapato ya fedha yake.
20
Mtumishi aliyekabidhiwa talanta tano akaja amechukua zile talanta tano faida,
akamwambia, `Bwana, ulinikabidhi talanta tano, hapa pana talanta tano zaidi
faida niliyopata.`
21 Bwana
wake akamwambia, `Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika
mambo madogo nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.`
22
"Mtumishi aliyekabidhiwa talanta mbili akaja, akatoa talanta mbili faida,
akisema, `Bwana, ulinikabidhi talanta mbili. Chukua talanta mbili zaidi faida niliyopata.`
23 Bwana
wake akamwambia, `Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika
mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.`
24
"Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaja, akasema, `Bwana, najua
wewe ni mtu mgumu; wewe huvuna pale ambapo hukupanda, na kukusanya pale ambapo
hukutawanya.
25
Niliogopa, nikaificha fedha yako katika ardhi. Chukua basi mali yako.`
26
"Bwana wake akamwambia, `Wewe ni mtumishi mwovu na mvivu! Unajua kuwa mimi
huvuna mahali ambapo sikupanda, na hukusanya pale ambapo sikutawanya.
27
Ilikupasa basi, kuiweka fedha yangu katika benki, nami ningelichukua mtaji
wangu na faida yake!
28 Basi,
mnyang`anyeni hiyo fedha mkampe yule mwenye talanta kumi.
29 Maana,
aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile
alicho nacho kitachukuliwa.
30 Na
kuhusu huyu mtumishi asiye na faida, mtupeni nje gizani! Huko kutakuwa na kilio
na kusaga meno.`
31
"Wakati Mwana wa Mtu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote
wakiwa pamoja naye, hapo ataketi juu ya kiti chake cha enzi kitukufu,
32 na
mataifa yote yatakusanyika mbele yake, naye atawatenganisha watu kama mchungaji
anavyotenganisha kondoo na mbuzi.
33
Atawaweka kondoo upande wake wa kulia na mbuzi upande wake wa kushoto.
34
"Kisha Mfalme atawaambia wale walio upande wake wa kulia, `Njoni enyi
mliobarikiwa na Baba yangu; pokeeni Ufalme mliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa
ulimwengu.
35 Maana
nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji;
nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha;
36
nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa
gerezani nanyi mkaja kunitembelea.`
37 Hapo,
hao watu wema watamjibu mfalme `Bwana, ni lini tulikuona mwenye njaa nasi
tukakupa chakula, au ukiwa na kiu nasi tukakunywesha maji?
38 Ni lini
tulikuona ukiwa mgeni nasi tukakukaribisha, au bila nguo nasi tukakuvika?
39 Ni lini
tulikuona ukiwa mgonjwa au mfungwa nasi tukaja kukutazama?`
40 Mfalme
atawajibu, `Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu
zangu wadogo, mlinitendea mimi.`
41
"Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, `Ondokeni mbele yangu
enyi mliolaaniwa! Nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa Ibilisi na
malaika wake.
42 Maana
nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi hamkunipa maji.
43
Nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi
hamkuja kunitazama.`
44
"Hapo nao watajibu, `Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, ukiwa
mgeni au bila nguo, ukiwa mgonjwa au mfungwa, nasi hatukuja kukuhudumia?`
45 Naye
atawajibu, `Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo
wa hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi.`
46 Basi,
hawa watakwenda kwenye adhabu ya milele, lakini wale waadilifu watakwenda
kwenye uzima wa milele."
|