Chapter 27
1 Kulipopambazuka, makuhani wakuu wote na wazee wa watu
walifanya mashauri juu ya Yesu wapate kumwua.
2 Wakamfunga pingu, wakamchukua, wakamkabidhi kwa Pilato,
mkuu wa mkoa.
3 Hapo, Yuda ambaye ndiye aliyemsaliti, alipoona kwamba
wamekwisha mhukumu Yesu, akajuta, akawarudishia makuhani wakuu zile sarafu
thelathini za fedha.
4 Akawaambia, "Nimekosa kwa kumtoa mtu asiye na hatia
auawe." Lakini wao wakasema, "Yatuhusu nini sisi? Hilo ni shauri
lako."
5 Naye akazitupa zile fedha Hekaluni, akatoka nje, akaenda
akajinyonga.
6 Makuhani wakuu wakazichukua zile fedha, wakasema,
"Haifai kuziweka katika hazina ya Hekalu kwa maana ni fedha za damu."
7 Basi, wakashauriana, wakazitumia kununua shamba la
mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni.
8 Ndiyo maana mpaka leo shamba hilo linaitwa Shamba la
Damu.
9 Hivyo maneno ya nabii Yeremia yakatimia:
"Walizichukua sarafu thelathini za fedha, thamani ya yule ambaye watu wa
Israeli walipanga bei,
10 wakanunua nazo shamba la mfinyanzi, kama Bwana
alivyoniagiza."
11 Yesu alisimamishwa mbele ya mkuu wa mkoa. Basi, mkuu wa
mkoa akamwuliza, "Je, wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?" Yesu
akamwambia, "Wewe umesema."
12 Lakini makuhani wakuu na wazee walipokuwa wanamshtaki,
hakujibu neno.
13 Hivyo Pilato akamwuliza, "Je, husikii mashtaka hayo
yote wanayotoa juu yako?"
14 Lakini Yesu hakumjibu hata neno moja; hata huyo mkuu wa
mkoa akashangaa sana.
15 Ilikuwa kawaida wakati wa Sikukuu ya Pasaka mkuu wa mkoa
kuwafungulia Wayahudi mfungwa mmoja waliyemtaka.
16 Wakati huo kulikuwa na mfungwa mmoja, jina lake Baraba.
17 Hivyo, watu walipokusanyika pamoja, Pilato akawauliza,
"Mwataka nimfungue yupi kati ya wawili hawa, Baraba*fq* ama Yesu aitwae
Kristo?"
18 Alisema hivyo maana alijua wazi kwamba walimleta kwake
kwa sababu ya wivu.
19 Pilato alipokuwa amekaa katika kiti cha hukumu, mke wake
akampelekea ujumbe: "Usijitie katika shauri la mtu huyu mwema, maana leo
nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake."
20 Lakini makuhani wakuu na wazee wakawashawishi watu
waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe.
21 Mkuu wa mkoa akawauliza, "Ni yupi kati ya hawa
wawili mnayetaka nimfungue?" Wakamjibu, "Baraba!"
22 Pilato akawauliza, "Sasa, nifanye nini na Yesu
aitwaye Kristo?" Wote wakasema, "Asulubiwe!"
23 Pilato akauliza, "Kwa nini? Amefanya kosa
gani?" Wao wakazidi kupaaza sauti: "Asulubiwe!"
24 Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na
kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule
umati wa watu, akasema, "Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri
lenu wenyewe."
25 Watu wote wakasema, "Damu yake na iwe juu yetu na
juu ya watoto wetu!"
26 Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, lakini
akamtoa Yesu asulubiwe.
27 Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya
ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima.
28 Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu.
29 Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani,
wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake,
wakamdhihaki wakisema, "Shikamoo mfalme wa Wayahudi!"
30 Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao
kichwani.
31 Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo
zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.
32 Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake
Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu.
33 Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake,
"Mahali pa Fuvu la kichwa,"
34 wakampa mchanganyiko wa divai na nyongo. Lakini Yesu
alipoonja akakataa kunywa.
35 Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa
kuyapigia kura.
36 Wakaketi, wakawa wanamchunga.
37 Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake
lilioandikwa, "Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi."
38 Wanyang`anyi wawili walisulubishwa pia pamoja naye,
mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia.
39 Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana
wakitikisa vichwa vyao na kusema,
40 "Wewe! Si ulijidai kulivunja Hekalu na kulijenga
kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi shuka
msalabani!"
41 Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na walimu wa
Sheria na wazee walimdhihaki wakisema,
42 "Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe
hawezi! Eti yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi
tutamwamini.
43 Alimtumainia Mungu na kusema eti yeye ni Mwana wa Mungu;
basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka."
44 Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye
wakamtukana.
45 Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, nchi yote ikawa
katika giza.
46 Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, "Eli,
Eli, lema sabakthani?" Maana yake, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona
umeniacha?"
47 Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema,
"Anamwita Eliya."
48 Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya
katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe.
49 Wengine wakasema, "Acha tuone kama Eliya anakuja
kumwokoa."
50 Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho.
51 Hapo pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu
mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;
52 makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa
wakafufuliwa;
53 nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini,
wakaingia katika Mji Mtakatifu, wakaonekana na watu wengi.
54 Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu
walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana,
wakasema, "Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu."
55 Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa
mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia.
56 Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao
Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo.
57 Ilipokuwa jioni, akaja mtu mmoja tajiri mwenyeji wa
Armathaya, jina lake Yosefu. Yeye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu.
58 Akamwendea Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Basi,
Pilato akaamuru apewe.
59 Yosefu akauchukua ule mwili akauzungushia sanda safi ya
kitani,
60 akauweka ndani ya kaburi lake jipya alilokuwa
amelichonga katika mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa
kaburi, akaenda zake.
61 Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwa wameketi
kulielekea kaburi.
62 Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalio,
makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato,
63 Wakasema, "Mheshimiwa, tunakumbuka kwamba yule
mdanganyifu alisema kabla ya kufa ati, `Baada ya siku tatu nitafufuka.`
64 Kwa hiyo amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu ili
wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu kwamba amefufuka. Uongo huu
wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa awali."
65 Pilato akawaambia, "Haya, mnao walinzi; nendeni
mkalinde kadiri mjuavyo."
66 Basi, wakaenda, wakalilinda kaburi, wakatia mhuri juu ya
lile jiwe na kuacha hapo askari walinzi.
|