Chapter 28
1 Baada ya Sabato, karibu na mapambazuko ya siku ile ya
Jumapili, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kutazama lile
kaburi.
2 Ghafla kutatokea tetemeko kubwa la nchi; malaika wa Bwana
alishuka kutoka mbinguni, akalivingirisha lile jiwe, akalikalia.
3 Alionekana kama umeme na mavazi yake yalikuwa meupe kama
theluji.
4 Walinzi wa lile kaburi wakatetemeka kwa hofu kubwa, hata
wakawa kama wamekufa.
5 Lakini yule malaika akawaambia wale wanawake, "Ninyi
msiogope! Najua kwamba mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa.
6 Hayupo hapa maana amefufuka kama alivyosema. Njoni mkaone
mahali alipokuwa amelala.
7 Basi, nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba
amefufuka kutoka wafu, na sasa anawatangulieni kule Galilaya; huko mtamwona.
Haya, mimi nimekwisha waambieni."
8 Wakiwa wenye hofu na furaha kubwa, hao wanawake walitoka
upesi kaburini, wakakimbia kwenda kuwaambia wanafunzi wake.
9 Mara,
Yesu akakutana nao, akawasalimu: "Salamu." Hao wanawake wakamwendea,
wakapiga magoti mbele yake, wakashika miguu yake.
10 Kisha
Yesu akawaambia, "Msiogope! Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende
Galilaya, na huko wataniona."
11 Wale
wanawake walipokuwa wanakwenda zao, baadhi ya walinzi wa lile kaburi walikwenda
mjini kutoa taarifa kwa makuhani wakuu juu ya mambo yote yaliyotukia.
12 Basi,
wakakutana pamoja na wazee, na baada ya kushauriana, wakawapa wale askari kiasi
kikubwa cha fedha
13
wakisema, "Ninyi mtasema hivi: `Wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba
sisi tukiwa tumelala.`
14 Na kama
mkuu wa mkoa akijua jambo hili, sisi tutasema naye na kuhakikisha kuwa ninyi
hamtapata matatizo."
15 Wale
walinzi wakazichukua zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Habari hiyo
imeenea kati ya Wayahudi mpaka leo.
16 Wale
wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya kwenye ule mlima aliowaagiza Yesu.
17
Walipomwona, wakamwabudu, ingawa wengine walikuwa na mashaka.
18 Yesu
akaja karibu, akawaambia, "Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.
19 Nendeni
basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu; mkiwabatiza kwa
jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.
20
Wafundisheni kushika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku
zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati."
|