Mark
Chapter 1
1 Habari
Njema ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.*fa*
2 Ilianza
kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: "Tazama, namtuma mjumbe
wangu akutangulie; yeye atakutayarishia njia yako.
3 Sauti ya
mtu imesikika jangwani: `Mtayarishieni Bwana njia yake, nyoosheni mapito
yake."`
4 Yohane Mbatizaji
alitokea jangwani, akahubiri kwamba ni lazima watu watubu na kubatizwa ili
Mungu awasamehe dhambi zao.
5 Watu
kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea,
wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani.
6 Yohane
alikuwa amevaa vazi lililofumwa kwa manyoya ya ngamia, na mkanda wa ngozi
kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni.
7 Naye
alihubiri akisema, "Baada yangu anakuja mwenye uwezo zaidi kuliko mimi,
ambaye mimi sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake.
8 Mimi
ninawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu."
9 Siku
hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane
katika mto Yordani.
10 Mara tu
alipotoka majini, aliona mbingu zimefunguliwa, na Roho akishuka juu yake kama
njiwa.
11 Sauti
ikasikika kutoka mbinguni: "Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa
nawe."
12 Mara
akaongozwa na Roho kwenda jangwani,
13 akakaa
huko siku arubaini akijaribiwa na Shetani. Alikuwa huko pamoja na wanyama wa
porini, nao malaika wakawa wanamtumikia.
14 Yohane
alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya
Mungu, akisema,
15
"Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari
Njema!"
16
Alipokuwa anapita kando ya ziwa Galilaya, aliwaona wavuvi wawili: Simoni na
Andrea ndugu yake wakivua samaki kwa wavu.
17 Yesu
akawaambia, "Nifuateni nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu."
18 Mara
wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.
19
Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Nao pia
walikuwa ndani ya mashua yao wakizitengeneza nyavu zao.
20 Yesu
akawaita mara, nao wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua pamoja na
wafanyakazi, wakamfuata.
21
Wakafika mjini Kafarnaumu, na mara ilipofika Sabato, Yesu akaingia katika
Sunagogi, akaanza kufundisha.
22 Watu
wote waliomsikia walishangazwa na mafundisho yake, maana hakuwa anafundisha
kama walimu wao wa Sheria, bali kama mtu mwenye mamlaka.
23 Mara
akatokea mle ndani ya sunagogi mtu mmoja mwenye pepo mchafu,
24 akapaaza sauti, "Una nini nasi, wewe Yesu wa
Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Najua wewe ni nani: wewe ni Mtakatifu wa
Mungu!"
25 Yesu
akamkemea, "Nyamaza! Mtoke mtu huyu."
26 Basi,
huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha akalia kwa sauti kubwa,
akamtoka.
27 Watu
wote wakashangaa, wakaulizana, "Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho
mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!"
28 Habari
za Yesu zikaenea upesi kila mahali katika wilaya ya Galilaya.
29
Wakatoka katika sunagogi, wakaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Simoni na
Andrea; Yakobo na Yohane walikwenda pamoja nao.
30 Basi, mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa kitandani ana
homa kali. Wakamwarifu Yesu mara alipowasili.
31 Yesu akamwendea huyo mama, akamshika mkono, akamwinua.
Na ile homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia.
32 Jioni, jua lilipokwisha tua, wakamletea Yesu wagonjwa
wote na watu waliopagawa na pepo.
33 Watu wote wa mji ule wakakusanyika nje ya mlango.
34 Naye Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa
mbalimbali; aliwafukuza pepo wengi, lakini hakuwaruhusu kusema kitu maana
walikuwa wanamjua yeye ni nani.
35 Kesho yake, kabla ya mapambazuko, Yesu alitoka, akaenda
mahali pa faragha kusali.
36 Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta.
37 Walipomwona wakamwambia, "Kila mtu
anakutafuta."
38 Yesu akawaambia, "Twendeni katika miji mingine ya
jirani nikahubiri huko pia, maana nimekuja kwa sababu hiyo."
39 Basi, akaenda kila mahali Galilaya akihubiri katika
masunagogi na kufukuza pepo.
40 Mtu mmoja mwenye ukoma alimwendea Yesu, akapiga magoti,
akamwomba, "Ukitaka, waweza kunitakasa!"
41 Yesu akamwonea huruma, akanyosha mkono wake, akamgusa na
kumwambia, "Nataka, takasika!"
42 Mara ukoma ukamwacha mtu huyo, akatakasika.
43 Kisha Yesu akamwambia aende zake upesi na kumwonya
vikali,
44 "Usimwambie mtu yeyote jambo hili, ila nenda
ukajionyeshe kwa kuhani; kisha utoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama
alivyoamuru Mose, iwe uthibitisho kwao kwamba umepona."
45 Lakini huyo mtu akaenda, akaanza kueneza habari hiyo
kila mahali na kusema mambo mengi hata Yesu hakuweza tena kuingia katika mji
wowote waziwazi; ikamlazimu kukaa nje, mahali pa faragha. Hata hivyo, watu
wakamwendea kutoka kila upande.
|