Chapter 2
1 Baada ya siku kadhaa, Yesu alirudi Kafarnaumu, watu
wakapata habari kwamba alikuwa nyumbani.
2 Basi, wakaja watu wengi sana hata nafasi yoyote
ikakosekana mlangoni. Yesu alikuwa akiwahubiria ujumbe wake,
3 wakati mtu mmoja aliyepooza alipoletwa kwake akiwa
amechukuliwa na watu wanne.
4 Kwa sababu ya huo umati wa watu, hawakuweza kumpeleka
karibu na Yesu. Basi, wakatoboa sehemu ya dari iliyokuwa juu ya mahali
alipokuwa Yesu. Walipokwisha pata nafasi, wakamteremsha huyo mtu akiwa amelala
juu ya mkeka.
5 Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza,
"Mwanangu, umesamehewa dhambi zako."
6 Baadhi ya walimu wa Sheria waliokuwa wameketi hapo
wakawaza mioyoni mwao,
7 "Anathubutuje kusema hivyo? Anamkufuru Mungu! Hakuna
mtu awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake."
8 Yesu alitambua mara mawazo yao, akawaambia, "Mbona
mnawaza hivyo mioyoni mwenu?
9 Ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia mtu huyu
aliyepooza, `Umesamehewa dhambi zako`, au kumwambia, `Inuka! Chukua mkeka wako
utembee?`
10 Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anayo mamlaka ya
kuwasamehe watu dhambi duniani." Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza,
11 "Nakwambia simama, chukua mkeka wako uende
nyumbani!"
12 Mara, watu wote wakiwa wanamtazama, huyo mtu akainuka,
akauchukua mkeka wake, akaenda zake. Watu wote wakashangaa na kumtukuza Mungu wakisema,
"Hatujapata kamwe kuona jambo kama hili."
13 Yesu alikwenda tena kando ya ziwa. Umati wa watu
ukamwendea, naye akaanza kuwafundisha.
14 Alipokuwa akipita, akamwona Lawi mwana wa Alfayo,
ameketi katika ofisi ya ushuru. Yesu akamwambia, "Nifuate!" Lawi
akasimama, akamfuata.
15 Baadaye, Yesu alikuwa amekaa mezani, nyumbani kwa Lawi,
kula chakula. Watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wamemfuata Yesu na
wengi wao wakawa wamekaa mezani pamoja naye na wanafunzi wake.
16 Basi, baadhi ya walimu wa Sheria ambao walikuwa
Mafarisayo walipomwona Yesu akila pamoja na watu wenye dhambi na watoza ushuru,
wakawauliza wanafunzi wake, "Kwa nini anakula pamoja na watoza ushuru na
wenye dhambi?"
17 Yesu alipowasikia, akawaambia, "Watu wenye afya
hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu
wema, ila wenye dhambi."
18 Wakati mmoja wanafunzi wa Yohane na wanafunzi wa
Mafarisayo walikuwa wanafunga. Basi, watu wakaja, wakamwuliza Yesu, "Kwa
nini wanafunzi wa Yohane na wa Mafarisayo wanafunga, lakini wanafunzi wako
hawafungi?"
19 Yesu akajibu, "Walioalikwa harusini wanawezaje
kufunga kama bwana harusi yupo pamoja nao? Wakati wote wawapo pamoja na bwana
harusi hawawezi kufunga.
20 Lakini wakati utafika ambapo bwana harusi ataondolewa
kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga.
21 "Hakuna mtu anayekata kiraka kutoka katika nguo
mpya na kukishonea katika nguo kuukuu. Kama akifanya hivyo, hicho kiraka kipya
kitararuka kutoka hilo vazi kuukuu, nalo litaharibika zaidi.
22 Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba
vikuukuu. Kama akifanya hivyo, divai itavipasua hivyo viriba, nayo divai pamoja
na hivyo viriba vitaharibika. Divai mpya hutiwa katika viriba vipya!"
23 Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika
mashamba ya ngano. Walipokuwa wanatembea, wanafunzi wake wakaanza kukwanyua
masuke ya ngano.
24 Mafarisayo wakawaambia, "Tazama! Kwa nini wanafanya
jambo ambalo si halali kufanya wakati wa Sabato?"
25 Yesu akawajibu, "Je, hamjapata kusoma juu ya kile
alichofanya Daudi wakati alipohitaji chakula? Yeye pamoja na wenzake waliona
njaa,
26 naye akaingia ndani ya Nyumba ya Mungu, akala ile mikate
iliyowekwa mbele ya Mungu. Jambo hili lilifanyika wakati Abiathari alikuwa
Kuhani Mkuu. Na ni makuhani tu peke yao waliokuwa wameruhusiwa kula mikate
hiyo. Lakini Daudi aliila, tena akawapa na wenzake."
27 Basi, Yesu akawaambia, "Sabato iliwekwa kwa ajili
ya binadamu na si binadamu kwa ajili ya Sabato!
28 Kwa hiyo, Mwana wa Mtu ni Bwana hata wa Sabato."
|