Chapter 3
1 Yesu aliingia tena katika sunagogi na mle ndani mlikuwa
na mtu aliyekuwa na mkono uliopooza.
2 Humo baadhi ya watu walimngojea amponye mtu huyo siku ya
sabato ili wapate kumshtaki.
3 Yesu akamwambia huyo mtu aliyekuwa na mkono uliopooza,
"Njoo hapa katikati."
4 Kisha, akawauliza, "Je, ni halali siku ya Sabato
kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuua?" Lakini
wao hawakusema neno.
5 Hapo akawatazama wote kwa hasira, akaona huzuni kwa
sababu ya ugumu wa mioyo yao. Kisha akamwambia huyo mtu, "Nyosha mkono
wako!" Naye akaunyosha mkono wake, ukawa mzima tena.
6 Mara Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri pamoja na
watu wa kikundi cha Herode jinsi ya kumwangamiza Yesu.
7 Yesu aliondoka hapo pamoja na wanafunzi wake, akaenda
kando ya ziwa, na umati wa watu ukamfuata. Watu hao walikuwa wametoka
Yerusalemu, Yudea,
8 Idumea, ng`ambo ya mto Yordani, Tiro na Sidoni. Watu hao
wengi walimwendea Yesu kwa sababu ya kusikia mambo mengi aliyokuwa ameyatenda.
9 Yesu akawaambia wanafunzi wake wamtayarishie mashua moja,
ili umati wa watu usije ukamsonga.
10 Alikuwa amewaponya watu wengi, na wagonjwa wote wakawa
wanamsonga ili wapate kumgusa.
11 Na watu waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu
walipomwona, walijitupa chini mbele yake na kupaaza sauti, "Wewe ni Mwana
wa Mungu!"
12 Lakini Yesu akawaamuru kwa ukali wasimjulishe kwa watu.
13 Yesu alipanda kilimani, akawaita wale aliowataka. Basi,
wakamwendea,
14 naye akawateua watu kumi na wawili ambao aliwaita
mitume,*fb* wakae naye, awatume kuhubiri
15 na wawe
na mamlaka ya kuwafukuza pepo.
16 Basi,
hao kumi na wawili walioteuliwa ndio hawa: Simoni (ambaye Yesu alimpa jina,
Petro),
17 Yakobo
na Yohane, wana wa Zebedayo (Yesu aliwapa hawa ndugu wawili jina Boanerge,
maana yake "wanangurumo"),
18 Andrea
na Filipo, Batholomayo, Mathayo, Thoma, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni
Mkanani na
19 Yuda
Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu.
20 Kisha
Yesu alikwenda nyumbani. Umati wa watu ukakusanyika tena, hata Yesu na wafuasi
wake wasiweze kupata nafasi ya kula chakula.
21 Basi,
watu wa jamaa yake walipopata habari hiyo wakatoka kwenda kumchukua maana
walikuwa wanasema kwamba amepatwa na wazimu.
22 Nao walimu
wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu, wakasema, "Ana Beelzebuli! Tena,
anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo."
23 Hapo
Yesu akawaita, akawaambia kwa mifano,"Shetani anawezaje kumfukuza Shetani?
24 Ikiwa
utawala mmoja umegawanyika makundimakundi yanayopigana, utawala huo hauwezi
kudumu.
25 Tena,
ikiwa jamaa moja imegawanyika makundimakundi yanayopingana, jamaa hiyo
itaangamia.
26 Ikiwa
basi, utawala wa Shetani umegawanyika vikundivikundi hauwezi kudumu, bali
utaangamia kabisa.
27
"Hakuna mtu awezaye kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang`anya
mali yake, isipokuwa kwanza amemfunga huyo mtu mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza
kumnyang`anya mali yake.
28
"Kweli nawaambieni, watu watasamehewa dhambi zao zote na kufuru zao zote;
29 lakini
anayesema mabaya dhidi ya Roho Mtakatifu, hatasamehewa kamwe; ana hatia ya
dhambi ya milele."
30 Yesu
alisema hivyo kwa sababu walikuwa wanasema, "Ana pepo mchafu.")
31 Mama
yake Yesu na ndugu zake walifika hapo, wakasimama nje, wakampelekea ujumbe
kutaka kumwona.
32 Umati
wa watu ulikuwa umekaa hapo kumzunguka. Basi, wakamwambia, "Mama yako na
ndugu zako wako nje, wanataka kukuona."
33 Yesu
akawaambia, "Mama yangu na ndugu zangu ni kina nani?"
34 Hapo
akawatazama watu waliokuwa wamemzunguka, akasema, "Tazameni! Hawa ndio mama
yangu na ndugu zangu.
35 Mtu
yeyote anayefanya anayotaka Mungu, huyo ndiye kaka yangu, dada yangu na mama
yangu."
|