Chapter 4
1 Yesu
alianza kufundisha tena akiwa kando ya ziwa. Umati mkubwa wa watu ulimzunguka
hata ikambidi aingie katika mashua na kuketi. Watu wakawa wamekaa katika nchi
kavu, kando ya ziwa.
2
Aliwafundisha mambo mengi kwa mifano, na katika mafundisho yake aliwaambia,
3
"Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu.
4
Alipokuwa akipanda, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila.
5 Nyingine
zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Mbegu hizo ziliota mara kwa
kuwa udongo haukuwa na kina.
6 Jua
lilipochomoza, zikachomeka; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu,
zikanyauka.
7 Nyingine
zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga, nazo hazikuzaa
nafaka.
8 Nyingine
zilianguka katika udongo mzuri, zikakua na kuzaa: moja punje thelathini, moja
sitini na nyingine mia."
9 Kisha
akawaambia, "Mwenye masikio na asikie!"
10 Yesu
alipokuwa peke yake, baadhi ya wale waliomsikia walimwendea pamoja na wale kumi
na wawili, wakamwuliza juu ya hiyo mifano.
11 Naye
akawaambia, "Ninyi mmejaliwa kujua siri ya Utawala wa Mungu, lakini wale
walio nje wataambiwa kila kitu kwa mifano,
12 ili, `Watazame kweli, lakini wasione. Wasikie kweli,
lakini wasielewe. La sivyo, wangemgeukia Mungu, naye angewasamehe."`
13 Basi, Yesu akawauliza, "Je, ninyi hamwelewi mfano
huu? Mtawezaje basi, kuelewa mfano wowote?
14 Mpanzi hupanda neno la Mungu.
15 Watu wengine ni kama wale walio njiani ambapo mbegu
zilianguka. Hawa hulisikia hilo neno lakini mara Shetani huja na kuliondoa neno
hilo lililopandwa ndani yao.
16 Watu wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa penye mawe.
Mara tu wanapolisikia hilo neno hulipokea kwa furaha.
17 Lakini haliwaingii na kuwa na mizizi ndani yao;
huendelea kulizingatia kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea
kwa sababu ya hilo neno mara wanakata tamaa.
18 Watu wengine ni kama zile mbegu zilizoanguka penye miti
ya miiba. Huo ni mfano wa wale wanaolisikia hilo neno,
19 lakini wasiwasi wa ulimwengu huu, anasa za mali na tamaa
za kila namna huwaingia na kulisonga hilo neno, nao hawazai matunda.
20 Lakini wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa katika
udongo mzuri. Hawa hulisikia hilo neno, wakalipokea, wakazaa matunda: wengine
thelathini, wengine sitini na wengine mia moja."
21 Yesu akaendelea kuwaambia, "Je, watu huwasha taa
wakaileta ndani na kuifunika kwa pishi au kuiweka mvunguni? La! Huiweka juu ya
kinara.
22 Basi, kila kilichofichwa kitafichuliwa, na kila
kilichofunikwa kitafunuliwa.
23 Mwenye
masikio na asikie!"
24
Akawaambia pia, "Sikilizeni kwa makini mnachosikia! Kipimo kilekile
mnachowapimia watu wengine, ndicho mtakachopimiwa; tena mtazidishiwa.
25 Aliye
na kitu atapewa zaidi; asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa."
26 Yesu
akaendelea kusema, "Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu
shambani.
27 Usiku
hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui
inavyofanyika.
28 Udongo wenyewe
huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: kwanza huchipua jani changa, kisha
suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke.
29 Nafaka
inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno
umefika."
30 Tena, Yesu
akasema, "Tuufananishe Utawala wa Mungu na nini? Tuueleze kwa mifano gani?
31 Ni kama
mbegu ya haradali ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote.
32 Lakini
ikisha pandwa, huota na kuwa mmea mkubwa kuliko mimea yote ya shambani. Matawi
yake huwa makubwa hata ndege wa angani huweza kujenga viota vyao katika kivuli
chake."
33 Yesu
aliwahubiria ujumbe wake kwa mifano mingine mingi ya namna hiyo; aliongea nao
kadiri walivyoweza kusikia.
34 Hakuongea
nao chochote bila kutumia mifano; lakini alipokuwa pamoja na wanafunzi wake
peke yao alikuwa akiwafafanulia kila kitu.
35 Jioni,
siku hiyohiyo, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, "Tuvuke ziwa, twende
ng`ambo."
36 Basi,
wakauacha ule umati wa watu, wakamchukua Yesu katika mashua alimokuwa.
Palikuwapo pia mashua nyingine hapo.
37 Basi,
dhoruba kali ikaanza kuvuma, mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikaanza kujaa
maji.
38 Yesu
alikuwa sehemu ya nyuma ya mashua, amelala juu ya mto. Basi, wanafunzi
wakamwamsha na kumwambia, "Mwalimu, je, hujali kwamba sisi
tunaangamia?"
39 Basi,
akaamka, akaukemea ule upepo na kuyaamrisha mawimbi ya ziwa, "Kimya!
Tulia!" Hapo upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa.
40 Kisha
Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Mbona mnaogopa? Je, bado hamna
imani?"
41 Nao
wakaogopa sana, wakawa wanaulizana, "Huyu ni nani basi, hata upepo na
mawimbi vinamtii?"
|