Chapter 5
1 Basi,
wakafika katika nchi ya Wagerase, ng`ambo ya ziwa.
2 Mara tu
Yesu aliposhuka mashuani, mtu mmoja aliyepagawa na pepo mchafu alitoka
makaburini, akakutana naye.
3 Mtu huyo
alikuwa akiishi makaburini wala hakuna mtu aliyeweza tena kumfunga kwa
minyororo.
4 Mara
nyingi walimfunga kwa pingu na minyororo lakini kila mara aliweza kuikata hiyo
minyororo na kuzivunja hizo pingu, wala hakuna mtu aliyeweza kumzuia.
5 Mchana
na usiku alikaa makaburini na milimani akipaaza sauti na kujikatakata kwa mawe.
6
Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akamwinamia
7 akisema
kwa sauti kubwa, "Una shauri gani nami, wewe Yesu Mwana wa Mungu aliye
juu? Kwa jina la Mungu, nakusihi usinitese!"
8 Alisema
hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, "Pepo mchafu, mtoke mtu
huyu.")
9 Basi,
Yesu akamwuliza, "Jina lako nani?" Naye akajibu, "Jina langu ni
`Jeshi`, maana sisi tu wengi."
10 Kisha
akamsihi Yesu asiwafukuze hao pepo katika nchi ile.
11
Kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe malishoni kwenye mteremko wa mlima.
12 Basi,
hao pepo wakamsihi, "Utupeleke kwa hao nguruwe, tuwaingie."
13 Naye
akawaruhusu. Basi, hao pepo wachafu wakatoka, wakawaingia wale nguruwe. Kundi
lote la nguruwe wapatao elfu mbili likaporomoka kwenye ule mteremko mkali mpaka
ziwani, likatumbukia majini.
14
Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakatangaza jambo hilo mjini na
mashambani. Watu wakafika kuona yaliyotukia.
15
Wakamwendea Yesu, wakamwona na mtu yuleyule aliyekuwa amepagawa na jeshi la
pepo ameketi chini, amevaa nguo na ana akili yake sawa, wakaogopa.
16 Watu
walishuhudia tukio hilo wakaeleza wengine mambo yaliyompata huyo mtu aliyekuwa
amepagawa na pepo na juu ya wale nguruwe.
17 Basi,
wakaanza kumwomba aondoke katika nchi yao.
18 Yesu
alipokuwa anapanda mashuani, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akamwomba
amruhusu kwenda naye.
19 Lakini Yesu akamkatalia. Badala yake akamwambia,
"Nenda nyumbani kwa jamaa yako, ukawaambie mambo yote Bwana aliyokutendea
na jinsi alivyokuonea huruma."
20 Basi, huyo mtu akaenda, akaanza kutangaza huko Dekapoli
mambo yote Yesu aliyomtendea; watu wote wakashangaa.
21 Yesu alivukia tena upande wa pili wa ziwa kwa mashua.
Umati mkubwa wa watu ukakusanyika mbele yake, naye akawa amesimama kando ya
ziwa.
22 Hapo akaja mmojawapo wa maofisa wa sunagogi, jina lake
Yairo. Alipomwona Yesu, akajitupa mbele ya miguu yake,
23 akamsihi akisema, "Binti yangu mdogo ni mgonjwa
karibu kufa. Twende tafadhali, ukamwekee mikono yako, apate kupona na
kuishi."
24 Basi, Yesu akaondoka pamoja naye. Watu wengi sana
wakamfuata, wakawa wanamsonga kila upande.
25 Mmojawapo alikuwa mwanamke mwenye ugonjwa wa kutokwa
damu kwa muda wa miaka kumi na miwili.
26 Mwanamke huyo alikuwa amekwisha sumbuka sana kuwaendea
waganga wengi. Na ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote, hakupata nafuu
bali hali yake ilizidi kuwa mbaya.
27 Alikuwa amesikia habari za Yesu, na hivyo akaupenya
msongamano wa watu kutoka nyuma, akagusa vazi lake.
28 Alifanya hivyo, maana alijisemea, "Nikigusa tu vazi
lake, nitapona."
29 Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, akajisikia mwilini
mwake kwamba ameponywa ugonjwa wake.
30 Yesu alitambua mara kwamba nguvu imemtoka. Basi
akaugeukia ule umati wa watu, akauliza, "Nani aliyegusa mavazi
yangu?"
31 Wanafunzi wake wakamjibu, "Unaona jinsi watu
wanavyokusonga; mbona wauliza nani aliyekugusa?"
32 Lakini Yesu akaendelea kutazama amwone huyo aliyefanya
hivyo.
33 Hapo huyo mwanamke, akifahamu yaliyompata, akajitokeza
akitetemeka kwa hofu, akajitupa chini mbele ya Yesu na kusema ukweli wote.
34 Yesu akamwambia, "Binti, imani yako imekuponya.
Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako."
35 Yesu alipokuwa bado anaongea, watu walifika kutoka
nyumbani kwa yule ofisa wa sunagogi, wakamwambia, "Binti yako amekwisha
kufa. Ya nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?"
36 Lakini, bila kujali walichosema, Yesu akamwambia mkuu wa
sunagogi, "Usiogope, amini tu."
37 Wala hakumruhusu mtu yeyote kufuatana naye ila Petro,
Yakobo na Yohane nduguye Yakobo.
38 Wakafika nyumbani kwa ofisa wa sunagogi naye Yesu
akasikia makelele, kilio na maombolezo mengi.
39 Akaingia ndani, akawaambia, "Mbona mnapiga kelele
na kulia? Msichana hakufa, amelala tu."
40 Lakini wao wakamcheka. Basi, akawaondoa wote nje,
akawachukua baba na mama ya huyo msichana na wale wanafunzi wake, wakaingia
chumbani alimokuwa huyo msichana.
41 Kisha akamshika mkono, akamwambia, "Talitha,
kumi," maana yake, "Msichana, nakwambia, amka!"
42 Mara msichana akasimama, akaanza kutembea. (Alikuwa na umri wa miaka kumi na
miwili.) Hapo watu wakashangaa kupita kiasi.
43 Yesu
akawakataza sana wasimjulishe mtu jambo hilo. Kisha akawaambia wampe huyo
msichana chakula.
|